• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Kiangazi: Serikali yaahidi kununua mifugo

Kiangazi: Serikali yaahidi kununua mifugo

Na GEOFFREY ONDIEKI

SERIKALI inalenga kuzindua mpango wa kuokoa mifugo katika maeneo yanayoathiriwa na ukame kama njia ya kupunguza athari za muda mrefu zinazosababishwa na janga hilo.

Wizara ya Ugatuzi ilisema kuwa hali inaendelea kuwa mbaya katika maeneo hayo huku mifugo zaidi wakitarajiwa kufa kutokana na ukosefu wa maji na lishe.

Akizungumza katika mkutano na wadau uliofanyika katika Mji wa Maralal, Kaunti ya Samburu, Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Abdul Bahari, alisema kuwa serikali itatafuta soko la mifugo kutoka kwa Kenya Meat Commission (KMC).

Alisema serikali iko tayari kununua mifugo dhaifu kutoka vijijini ili kuwaokoa wafugaji kutokana na hasara wanayopata kufuatia ukame huo.

“Mpango huo unalenga kuwaokoa wafugaji kutoka maeneo yaliyoathiriwa na ukame. Tutanunua mifugo kutoka vijiji mbalimbali na kuwatafutia soko wafugaji hao.”

Bw Bahari alisema zoezi hilo linalenga kuwachukua mifugo dhaifu kwa kununua ng’ombe, mbuzi na kondoo kutoka kwa wafugaji watakaokubali. Mifugo itakayonunuliwa itatumika kama chakula na kusambazwa kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi.

Serikali pia inalenga kusambaza msaada wa chakula na lishe ya mifugo katika kaunti 10 zilizoathiriwa na ukame.Alisema tayari magunia 8,000 ya lishe ya mifugo yametumwa katika kaunti hizo.

Kando na lishe ya mifugo, wizara hiyo pia inatoa msaada wa pesa na chanjo kwa familia zilizoathiriwa.Bw Bahari alisema wanalenga familia zilizo katika mazingira magumu katika kaunti 10 zilizoathirika zaidi miongoni zikiwa za Samburu, Marsabit, Isiolo, Mandera na Turkana.

Kulingana na Mamlaka ya Kufuatilia Hali ya Ukame nchini (NDMA), Kaunti zaidi ya 10 kaskazini mwa Kenya zinaendelea kushuhudia ukame jambo linalosababisha ugumu wa kupata chakula, maji na malisho ya mifugo.

Mamlaka hiyo imesema kuwa uzalishaji wa maziwa na nyama kutoka kaunti mbalimbali za wafugaji umeshuka kufuatia kupungua kwa malisho kkutokana na ukosefu wa mvua.

Asilimia kubwa ya wakazi wa kaunti kame huendesha ufugaji na kawaida na hutegemea mifugo kwa mahitaji yote ya kimsingi.

Wakazi hawa imebainika huathiriwa mno na vifo vya mifugo kwa sababu ndio tegemeo lao kujisaidia kiuchumi.Baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wanashindwa kujimudu kimaisha.

Bei ya mifugo imeshuka huku baadhi ya masoko yakifungwa kutokana na ukosefu wa wanunuzi.

You can share this post!

UFISADI: Wazito sasa wafinywa

AG aanza rasmi juhudi za kuokoa BBI