• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Kibarua ashtakiwa kwa kuvunja vioo vya madirisha ya kituo cha polisi

Kibarua ashtakiwa kwa kuvunja vioo vya madirisha ya kituo cha polisi

NA RICHARD MUNGUTI

KIBARUA ameshtakiwa kuvunja vioo vya madirisha 17 katika kituo kidogo cha polisi cha Ngara kwa kuvipiga mawe baada ya afisa mmoja wa polisi kumtusi mkewe kwa kumwita malaya.

Leo Jumanne ameomba kesi hiyo ipelekwe mahakama kuu akatetee haki za mpenzi wake.

Justine Onami Osinde aliyefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Wandia Nyamu alisema “ninataka mahakama kuu iamue ikiwa polisi ana idhini ya kumtusi mke wangu na kutaka wacheze densi naye.”

Mshtakiwa alieleza korti ni haki yake kupata ufafanuzi chini ya sheria za kitengo cha haki kwa wananchi.

Aliposomewa shtaka la kuharibu mali ya serikali, Osinde aliambia hakimu: “Nilipandwa na mori afisa wa polisi alipomtukana mke wangu kwa kudai alikuwa malaya.”

Mshtakiwa alieza korti hakunuia kuzua vurugu lakini ilibidi amtetee mkewe dhidi ya matusi kutoka kwa afisa huyo wa usalama.

Mahakama ilielezwa mshtakiwa alichokozana na afisa katika kilabu kimoja ambapo Osinde na mkewe walikuwa wameenda kukodisha chumba cha kulala baada ya kufungiwa nyumba na ladilodi.

Afisa huyo alimtaka wacheze rumba na mke wa mshtakiwa ndipo vurugu ikatokea.

Mkewe mshtakiwa alikataa ombi la afiswa huyo wa polisi ndipo akaanza kumtusi.

Mzozo ulizuka kisha mshtakiwa akamtandika sumbwi afisa huyo wa polisi.

Papo hapo maafisa wengine wa polisi waliokuwa wamevaa kiraia waliingilia patashika hiyo na kumkamata Osinde.

Alitiwa pingu na kupelekwa kituo kidogo cha polisi cha Ngara ambapo alivunjavunja vioo vya madirisha.

“Naomba hii mahakama inipe fursa ya kuwasilisha kesi katika mahakama kuu kutetea haki zangu,” Osinde alimsihi hakimu.

Bw Osinde aliendelea kusema anataka mahakama kuu ifafanue ikiwa haki zake zilikandamizwa na polisi waliomtia mbaroni kwa kumzuia afisa wa polisi akimchukua mkewe Osinde kwa nguvu wacheze densi.

“Nataka mahakama kuu iamue kesi hii kujua ikiwa ni ukiukaji wa sheria kumtetea mke wangu dhidi ya dhuluma za polisi,” Osinde alieleza hakimu.

Bi Wandia alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh20,000 kumwezesha kuwasilisha kesi mahakama kuu kufafanuliwa haki zake.

  • Tags

You can share this post!

Montreal anayochezea Wanyama yaona cha mtema kuni dhidi ya...

Kabando adai ubaguzi ndani ya Azimio Nyeri

T L