• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kinaya Nairobi ikipanga kununua maboti kudhibiti athari za El Nino

Kinaya Nairobi ikipanga kununua maboti kudhibiti athari za El Nino

NA WINNIE ONYANDO

NI kinaya kuwa serikali ya Kaunti ya Nairobi inapanga kununua maboti yanayoweza kuruka hewani ili kusaidia kukabiliana na athari za mvua ya El Nino inayotarajiwa kuanza wakati wowote.

Kulingana na Bramwel Simiyu, Mwenyekiti wa jopokazi la El Niño katika Kaunti ya Nairobi, kaunti inakadiria kutumia angalau Sh1 bilioni katika kupunguza athari za mvua ya El Niño.

“Lazima pia tujiandae kukabiliana na El Niño, inapotokea lazima tuwe na ambulensi, magari ya zimamoto, maboti ya injini yanayoweza kuruka hewani,” Bw Simiyu akasema.

Hiki ni kinaya kwa sababu mara nyingi Kaunti ya Nairobi haijawahi kupata mvua kiasi kwamba wakazi wanatumia boti.

Serikali ya Kaunti pia imekuwa na shughuli nyingi katika kuchora ramani za maeneo ambayo huenda yakaathiriwa pakubwa na El Nino.

“Kuna hatari. Kaunti ya Nairobi ina maeneo 500 ambayo ni hatari,” Simiyu alisema.

Kadhalika, Simiyu alisema wamebaini makazi mbadala kwa wale wanaoishi kwenye maeneo ambayo huenda yakaathiriwa na mafuriko.

Mojawapo ya makazi kama haya ni Ukumbi wa Joseph Kang’ethe huko Kibra.

“Tutatoa chakula, mahema, na blanketi kwa waathiriwa,” akasema.

Kutokana na hatari inayojiri, kaunti pia imetoa wito kwa watu wanaoishi kando au kwenye maeneo hatari kuhama mapema.

Kando na hayo, Simiyu alifichua kuwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi inapanga kujenga nyumba za bei nafuu kwa wale walio kwenye maeneo hatari na imetenga eneo la Dagorreti Corner na kando ya barabara ya Jogoo Rd na eneo la Eastlands.

Kuhusu kujitayarisha kuzuia maafa wakati wa El Niño, Simiyu alisema kuwa serikali ya kaunti iko mbioni kununua maboti kabla ya El Niño kuanza katika muda wa wiki moja ijayo kando na kutoa usaidizi wa kisaikolojia na ushauri kwa watakaoathiriwa.

  • Tags

You can share this post!

Nashindwa kuambia mke wangu dadake ni mkora, huenda...

Zari amtia wivu Diamond kwa kuolewa na...

T L