• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kinaya wakazi majirani wa bomba kuu kukosa maji safi

Kinaya wakazi majirani wa bomba kuu kukosa maji safi

JURGEN NAMBEKA Na MAUREEN ONGALA

KATIKA kijiji cha Lango Baya, Kaunti ya Kilifi, wakazi wanapitia hali ngumu kupata maji safi licha ya kuwa wanapakana na bomba kuu la usambazaji maji safi la Baricho.

Kwa kuishi karibu na bomba hilo, wengi wangetarajia kuwa wakazi hao wangepewa kipaumbele kupata maji safi kwa urahisi.

Kinaya ni kuwa, wakati asasi husika zinaposambaza zaidi ya lita milioni 90 za maji kila siku kwa miji ya Kilifi, Malindi na Kaunti ya Mombasa kutoka kwa bomba hilo kuu, wanakijiji hao hubaki wakitumia maji ya mtoni au kununua ya visimani.

Masaibu hayo ya wakazi wa Lango Baya yanadhihirisha kuwa, ujenzi wa miundomsingi pekee inayogharimu mabilioni ya pesa haitoshi kuupa umma afueni.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha kuwa, umaskini umewazuia wanakijiji kugharimia malipo ya kuunganisha mabomba ya maji hadi nyumbani kwao.

Wale wachache waliofanikiwa kugharimia hayo huwauzia wenzao, ambapo mtungi wa lita 20 huuzwa Sh5 na wengine wakiuza mitungi mitatu kwa Sh10.

Licha ya hayo, wanakijiji wengi bado hawamudu kununua maji hayo kila siku wakiamua kutumia maji ya visima au yale ya Mto Galana.

Bw Johann Kithi, ambaye ni mkulima, achimbua udongo kupata maji ya kunywa karibu na Mto Galana. PICHA | WACHIRA MWANGI

Mkulima Johann Kithi, ambaye anafanya kilimo cha kunyunyizia maji kando ya Mto Galana anasema kwamba idadi ya kina mama wanaofika kisiwani kuteka maji asubuhi huwa kubwa sana.

“Kila siku nikija Mto Galana huwa ninawakuta kina mama wakichota maji. Watu wamevuta maji ambayo wanayauza lakini wakati mwingine unapiga hesabu iwapo utanunua unga au maji. Kwa hivyo, wao hununua unga wa mahindi kisha maji wao hutumia haya,” anasema Bw Kithi, akiwa mtoni.

Mhudumu wa bodaboda akipita palipo na bomba la maji. PICHA | WACHIRA MWANGI

Kwa mtazamo wake, licha ya mabomba kupita karibu na nyumbani kwake, pia yeye hana uwezo wa kugharimia bei ya kuyaunganisha hadi nyumbani.

“Bomba la maji limepita nyuma ya nyumba yetu. Tulimwita fundi akaja kutupa makadirio ya kuvuta maji na akatueleza tujiandae na Sh35,000 ambayo ni ghali sana,” anaeleza Bw Kithi.

Mbali na ada za kuunganisha maji, pia wao hukadiria ada watakazotakikana kulipa kila mwezi.

Mkazi mwingine, Bi Jacinta Charo, anasema kuwa, licha ya kuwepo maji yanayouzwa Sh10 kwa mitungi mitatu ya lita 20, wakati mwingine pesa hizo hazipatikani.

“Wakazi wa Lango Baya huishia kuchota maji kwenye mashimo madogo yaliyochimbwa kando ya mto. Tumezoea kuyatumia maji hayo hivyo tu,” akasema Bi Charo.

Maelezo sawa na hayo yalitolewa na mkazi mwingine wa eneo hilo, Bw Dan Mwaro, anayeishi na familia yake.

Kwa miaka mingi sasa, suala la uhaba wa maji limekuwa likitajwa na viongozi wa Kilifi kama linalohitaji kusuluhishwa kwa dharura.

Wiki iliyopita, gavana Gideon Mung’aro, alihakikishia wakazi kwamba atajitolea kutimiza ahadi yake kwa wakazi kuhusu kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa maji wa Bamba-Mnagoni-Midoina-Ndharako, eneobunge la Ganze, Bw Mung’aro alisema atashirikiana kwa karibu na serikali ya kitaifa ili kuboresha miundomsingi ya maji katika Kaunti ya Kilifi.

“Niliahidi kwamba tatizo la maji litakuwa historia Kilifi na lazima nitimize ahadi hiyo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wawakilishi Kenya Kwanza watakaoshiriki maelewano na Azimio

Wahudumu wa mochari wafutwa kazi

T L