• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kindiki atekeleza mabadiliko tata ya kiutawala Murang’a

Kindiki atekeleza mabadiliko tata ya kiutawala Murang’a

NA MWANGI MUIRURI

MKUU wa kaunti ndogo ya Ithanga/Kakuzi Bi Angela Mutindi Makau ambaye anatuhumiwa kwa wizi wa mitambo ya miale ya jua ya kufaa wenyeji kupata maji safi amehamishwa ahudumu katika makao makuu ya wizara.

Kanuni za huduma ni kwamba washukiwa wote kwanza wasimamishwe kwa muda ili kupisha uchunguzi na kisha wakifunguliwa mashtaka wasimamishwe kazi kisha wafutwe wakihukumiwa au warejee wakiondolewa lawama.

Mnamo Mei 10, 2023, iliripotiwa kwamba maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walivamia nyumba yake katika Kaunti ya Machakos na kutwaa mitambo 13 na operesheni hiyo ikanakiliwa katika kitabu cha matukio (OB) katika kituo cha polisi cha Kirwara kama kisa: OB  23/10/5/2023.

Aliyekuwa Naibu Kamishna wa Ithanga/Kakuzi Bi Angela Makau ambaye anatuhumiwa kuiba mitambo ya miale ya jua ya kusaidia wenyeji kupata maji safi. Amehamishiwa hadi makao makuu ya kiutawala ya Harambee House. PICHA | MWANGI MUIRURI

Baada ya kesi yake kukwama na pia yeye kubakia afisini, mnamo Ijumaa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki alitoa taarifa ya kuonyesha afisa huyo akipewa uhamisho hadi makao makuu ya wizara huku Bw Peter Ndungu Gicheha akijaza pengo lake. Bw Gicheha alikuwa akihudumu katika kaunti ndogo ya Mathira Mashariki.

Kwa sasa, Rais wa Muungano wa Mawakili Nchini (LSK) tawi la Murang’a Bw Alex Ndegwa amesema kuwa anafuatilia kesi hiyo ambayo faili yake imekwama katika afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).

“Tangu faili hiyo ifunguliwe na kutumwa ikiwa na ushahidi katika afisi ya DPP haijarejeshwa kwa DCI ili wafungue mashtaka au wazidishe uchunguzi. LSK hapa Murang’a tunaifuatilia,” akasema.

Katika kisa kingine cha butwaa, mkuu wa kaunti ndogo ya Murang’a Kusini ambaye alifurushwa na kuteremshwa mamlaka mwaka 2022 Bw Mawira Mungania, amerejeshewa wadhifa wake.

Bw Mungania alihamishiwa eneo la Kaskazini Mashariki akiwa msaidizi wa mkuu wa eneo (RC) lakini sasa Bw Kindiki amemrejesha katika eneo la Murang’a Kusini akiwa Naibu Kamishna.

Bw Mungania amechukua nafasi ya Bw Gitonga Murungi ambaye anasifiwa na wenyeji kwa kudhalalisha umang’aa na ujeuri wa wauzaji vileo na mihadarati na kuimarisha hali ya Usalama wa mitaa hatari kama Maragua, Gakoigo, Gikindu na Samar.

Akitolewa eneo hilo, aliyekuwa mshirikishi wa eneo la Kati Bw Wilfred Nyagwanga alisema kwamba “Bw Mungania alihusishwa na maandalizi haramu ya kikao cha bodi ya mashamba”.

Kwa sasa, Bw Mungania anarejea katika eneo ambalo kwa sasa linashuhudia vita dhidi ya baa haramu na magenge ya utekaji nyara.

Bw Murungi amehamishwa hadi kaunti ndogo ya Kabete.

Mwingine ambaye amelengwa katika uhamisho huo ni Naibu Kamishna wa Kigumo ambaye alikuwa Bw Stanslaus Apwokha.

Eneo la Kigumo limekuwa likimulikwa kufuatia visa vya ukora wa watengenezaji wa pombe haramu, wamiliki wa baa, wezi wa mavuno, wizi wa mifugo na uchezaji kamari.

Wakulima wamekuwa wakichukua sheria mkononi kwa kuwaua washukiwa wa wizi wa mifugo na mimea huku nao wanaume wakielezea wasiwasi wao kuhusu magenge ya ulawiti.

Nafasi ya Bw Apwokha itachukuliwa na Bw Buxton Abwasi Mayabi aliyehamishwa kutoka kaunti ndogo ya Trans Mara Mashariki.

Naye Bw Musa Kimomo Okango amehamishwa kutoka Murang’a alikohudumu kama msaidizi wa Kamishna wa Kaunti hadi eneo la Khorof Harar.

  • Tags

You can share this post!

Mabilionea waangamia wakizuru meli iliyozama

Pasta Ezekiel aandaa maombi maalum kubariki tawi jipya

T L