• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 8:55 AM
Kingi aonya maafisa

Kingi aonya maafisa

Na MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi ameonya wafanyakazi wa kaunti dhidi ya kujaribu kuvuruga mfumo mpya wa ulipaji ada kidijitali ulionuiwa kukomesha ufisadi na wizi wa pesa za umma.

Akizungumza wakati wa kuzindua mfumo mpya wa kukusanya malipo ya ada za ardhi na ujenzi kidijitali, Bw Kingi alisema tekinolojia hiyo itarahisisha pia uwezo wa kaunti kutambua watumishi wa umma walio watepetevu katika kazi zao.

“Mfumo huu utaziba mwanya ambao watu walikuwa wakitumia kufuja pesa. Tunawalipa mishahara, tumieni pesa tunazowalipa kufanya chochote kile mtakacho. Tusisikie kuwa huu mpango unapigwa vita kwa sababu umeziba mwanya mliokuwa mkitumia kupata pesa kwa njia haramu,” akasema.

Kando na kusaidia kaunti kuongeza mapato yake, mfumo huo pia umenuiwa kuwezesha utoaji huduma kwa haraka kwa manufaa ya waekezaji.Bw Kingi alisisitiza kuwa kaunti yoyote ile inayolenga kuvutia waekezaji ni lazima iwe na uwezo wa kutoa huduma haraka na kwa uwazi.

“Mwekezaji huyo huyo tunayehangaisha ambaye anategemewa kujenga kiwanda ambacho kitaajiri zaidi ya vijana 10,000 Kilifi atapeleka kiwanda chake kwingine kwa sababu ya afisa mmoja mlafi,” akasema.Waziri wa Fedha katika kaunti hiyo, Bw Nzai Kombe, alisema utafiti wa Wizara ya Fedha ilibainisha kuwa Kilifi ina uwezo wa kukusanya takriban Sh2 bilioni kwa mwaka.

Hata hivyo, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa kaunti hiyo ilikuwa Sh800 milioni pekee katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge ataka Magoha ahojiwe kuhusu karo

Wakenya KPA wafundisha klabu za Malawi jinsi ya kucheza...