• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Kioja Gachagua akimsalimu Raila baada ya kuapa awali kutofanya hivyo

Kioja Gachagua akimsalimu Raila baada ya kuapa awali kutofanya hivyo

Na WANGU KANURI

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua alikiuka ‘kiapo’ chake baada ya kumsalimu kiongozi wa Azimio Raila Odinga kwa mkono Septemba 5, 2023.

Bw Odinga aliyefika katika Kongamano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi linaloendelea katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) alisalimiwa kwa tabasamu kubwa kutoka kwa Bw Gachagua.

Wawili hao walionaswa kwenye video, nyuso zao zilionyesha furaha kubwa huku wakinong’onezeana. Baadaye, Bw Gachagua alionekana akimwonyesha njia Bw Odinga.

Hata hivyo, miezi kadhaa iliyopita Bw Gachagua aliapa kutomsalimu Bw Odinga katu.

Akizungumzia wakazi wa Kiambu katika kanisa la African Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA), Bw Gachagua alisema, “Rais Ruto alitueleza hapo awali kuwa angemuomba Bw Odinga asitishe maandamano na kufanya mazungumzo nao na nikaafikiana naye. Bw Odinga sasa anasema kuwa hataki handisheki na mimi. Mimi ninaonekana kama mtu ambaye angependa kumsalimia kwa mkono?”

Kisha akaongeza, “Bw Odinga ana tabia ya kubadilisha watu. Alimbadilisha mtoto wetu, Uhuru Kenyatta. Rais huyo wa zamani alikuwa mzuri mpaka Bw Odinga alipoingia kwenye serikali yake. Unaweza kuwa na handisheki naye kisha mambo yaende mrama. Niambieni mnaweza niruhusu kuwa na handisheki na yeye? Siwezi mimi sitakuwepo. Mimi ni mume wa mhubiri.”

Kabla ya matamshi ya naibu huyo wa rais, Bw Odinga alikuwa amehutubia wananchi akisema kuwa hatamani kumsalimu Bw Gachagua.

“Hatujawahi kuzungumzia mambo ya handisheki. Hayo maneno yanatoka tu upande huo na ni wao wamekuwa wakisema kuwa tunataka handisheki au serikali ya nusu mkate. Ambieni Bw Gachagua, sitaki hata kumsalimia kwa mkono,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Beldine Odemba ataja wachezaji 30 wa kuwinda tiketi...

Rais Ruto amuomboleza Muthoni wa Kirima kama shujaa...

T L