• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Korti yamwacha Mackenzie kwa mataa

Korti yamwacha Mackenzie kwa mataa

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mkuu wa vifo vya mamia ya watu vilivyotokea katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Bw Paul Mackenzie, ameachwa kwa mataa baada ya mahakama kujitenga na uchunguzi uliokuwa ukiendelezwa na kamati maalumu ya Seneti.

Wiki iliyopita, kamati hiyo ilimtaka Bw Mackenzie kufika mbele yake jijini Nairobi lakini wakili wake, Bw Wycliffe Makasembo, akaomba mwezi mmoja zaidi ili wajiandae.

Kamati hiyo ilionya kuwa, watu ambao wanakaidi amri ya kufika mbele yao watachukuliwa hatua za kisheria.

Jana, Bw Makasembo aliiomba mahakama hiyo kuzuia Seneti kumwita na kumhoji Bw Mackenzie.

Wakili huyo alisema mchakato wa mahakama unapaswa kuruhusiwa kuendelea bila kesi sawia na hiyo katika jukwaa lingine.
Kulingana na Bw Makasembo, Mackenzie ‘angejichongea’ kama angefika mbele ya Seneti kujibu maswali kuhusu matukio ya Shakahola kabla ya kesi yake kukamilika.

“Je, kamati ya Seneti ina mamlaka ya kuchunguza mashtaka ya mauaji nchini? Tunaomba mahakama itoe mwongozo kuhusu kesi hizi sawia,” akasema Makasembo, akidai shughuli za kamati hiyo ni sawa na serikali kuingilia kazi za mahakama.

Hata hivyo, Mahakama ilijitenga na uchunguzi wa Seneti kuhusu maafa ya Shakahola.

Hakimu Mwandamizi Mkuu Yusuf Shikanda alisema kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kuzuia Kamati ya Seneti kumwita na kumhoji Mackenzie kuhusu mauaji ya Shakahola.

“Siwezi kuzuia Seneti kumhoji Mackenzie kwani sifanyi kazi huko,” akasema hakimu.

Badala yake, Bw Shikanda alimshauri Mackenzie na washukiwa wenzake kuandama njia nyingine za kisheria ikiwa wanaamini kuwa Seneti imekiuka haki zao kwa kutoa wito huo.

Zaidi ya hayo, hakimu huyo alifafanua kuwa mahakama yake haiwezi kuelekeza shuguli za Seneti kwani jukumu hilo litakuwa nje ya mamlaka yake.

“Sitakiwi kujibu suala lolote kuhusu ufanyakazi wao kwa hivyo siwezi kutoa maelekezo zaidi. Wahojiwa wanaweza kuweka ombi hilo kwenye jukwaa linalofaa,” alisema Bw Shikanda.

Mackenzie ameelezea wasiwasi wake kuwa serikali imemlenga kwa njia isiyozingatia haki tangu alipokamatwa Aprili mwaka huu.

Alisikitika kuwa viongozi wakuu wa serikali wamekuwa wakitoa vitisho ambavyo vimemfanya aingiwe na hofu kuhusu hatma ya kesi yake kwani serikali “ishafanya uamuzi wake hata kabla ya kufunguliwa mashtaka rasmi”.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina, pia hakujibu hoja za Mackenzie, akieleza kuwa hana maelekezo ya kuzungumzia suala hilo.

Jumatatu, Mackenzie aliitaka kamati hiyo kumpa angalau mwezi mmoja kufika mbele yake kuhojiwa. Alilalamika kwamba alipewa notisi fupi ya kujiwasilisha, ambayo pia ilitolewa bila kushauriwa.

Serikali imeomba kuongezewa muda hadi miezi sita ili kuwazuilia Mackenzie na wenzake huku upelelezi ukiendelea.

Mackenzie na washirika wake bado hawajawashilisha jibu kwa ombi hili. Mahakama pia imefahamishwa kuwa uchunguzi wa kijamii kuhusu Mackenzie na washirika wake umekamilika.

Ripoti hiyo iliwasilishwa mahakamani huku hakimu akielekeza kuwa inapaswa kuwa siri baina ya washukiwa, mahakama na upande wa mashtaka. Kesi hiyo itatajwa Novemba 9.

  • Tags

You can share this post!

Magavana wataka Inspekta Jenerali amuombe Mwangaza radhi...

Aliniacha akaolewa, sasa anataka tuoane baada ya kuachana...

T L