• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
KTDA: Bonasi ya chai kuchelewa

KTDA: Bonasi ya chai kuchelewa

NA MWANGI MUIRURI

WAKUZAJI wa majanchai nchini wameambiwa wasubiri hadi Oktoba 2023 kupokea bonasi kinyume na vile wamekuwa wakiipata mwezi wa Juni kila mwaka.

Mwenyekiti wa shirika la ustawishaji wa kilimo cha majanichai nchini – Kenya Tea Development Agency (KTDA) – Bw David Ichoho mnamo Julai 4, 2023 akihojiwa na kituo cha runinga cha Inooro amesema kwamba bonasi hiyo italipwa sambamba na mavuno ya Septemba.

Mwaka 2022, malipo ya bonasi yaliingizwa siasa ambapo yalilipwa mwezi wa sita huku kukiwa na majanichai ya miezi mitatu ambayo hayakuwa yameuzwa.

Ikizingatiwa kwamba bonasi hulipwa baada ya hesabu za mauzo za ujumla wa miezi 12, hatua hiyo ya serikali ya kulipa kutokana na hesabu za miezi saba ilimaanisha ukadiriaji wa kukadiria na kwa kuwa hakukuwa na pesa, serikali ikilenga siasa za uchaguzi ilikopa na ikalipa kiwango cha juu.

Mkopo huo ulisababisha malipo ya bonasi ndogo kupunguka na pia unasemwa na wadadisi kuwa kiini cha kusukumwa kwa bonasi kuu hadi Oktoba.

“Tunataka kuweka wazi hesabu zetu, tuzilainishe na kisha ukadiriaji wa bonasi uwe wa uhakika na unaozingatia hesabu halisi za mavuno, mauzo na gharama,” akasema Bw Ichoho.

Amefafanua kwamba bonasi itakayolipwa wakati huu itakuwa nono na ya kupendeza “licha ya kuwa tulikumbana na athari hasi za kimazingira zilizotutwika ukame ambao ulikuwa haujawahi kushuhudiwa katika maeneo ya ukuzaji wa majanichai”.

Amesema ukame huo ulikausha chemchemi za maji nchini kiasi cha kudunisha mavuno lakini “Mungu akawa mwema kwetu kwa kuwa pato sokoni liliimarika”.

Amesema lengo kuu la sasa ni kuimarisha pato kwa mkulima awe akitia mfukoni asilimia 80 ya mauzo jumla.

“Kwa sasa tuko katika kiwango cha asilimia 75 na kabla ya mwaka huu kuisha, tunatazamia nyongeza nyingine ya asilimia tano kwa manufaa ya mkulima. Hii ina maana kwamba wafanyakazi wetu wote watahitajika kupoteza hata marupurupu na wengine wapoteze asilimia za mishahara kwa kuwa kipaumbele ni mkulima,” akasema.

Aidha, ameonya kwamba wakulima ambao wanachuuza majanichai yao kwa madalali huenda wapigwe marufuku ya kuwa chini ya udhibiti wa KTDA.

“Hatuwezi kuwa sisi ndio tunawapa fatalaiza, kuwalipia wakurugenzi mishahara na hatimaye kuweka miundombinu ya soko kisha mavuno yakifika mnayachuuza kwa madalali. Tutawatema ili mjipange kivyenu,” akatishia.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro atishia kuwatimua vibarua kwa kugeuka...

Mackenzie aomba mlo spesheli kizuizini

T L