• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
Kumbe maseneta ni wabwekaji wasio na uwezo kung’ata!

Kumbe maseneta ni wabwekaji wasio na uwezo kung’ata!

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta ambao walikuwa wakipiga domo wakitisha kuangusha Mswada wa BBI wameibuka kuwa wabwekaji wasio na uwezo wa kuuma.

Kabla ya kura hiyo, wanasiasa hao, wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, walidai kuwa mswada huo ulikuwa kasoro kadha na vipengele vinavyokiuka katiba.

Hatimaye walipiga kura ya kuupitisha.Wiki jana wakati wa mjadala kuhusu mswada huo katika seneti, Bw Orengo alichemka kwa hasira akiwakaripia watu aliodai walijaribu kumwelekeza namna ya kuendesha majukumu yake kama seneta.

Alishikilia kuwa angeendelea kushinikiza mswada huo ufanyiwe marekebisho bila kuogopa yeyote.“Sijawahi kutishwa tangu nilipoingia katika siasa, kwa sababu nimewaona watu wenye mamlaka wakija na kuondoka.

Nimewaona marais wakija na kuondoka” akafoka.Alitaja Seneti kama bunge muhimu lenye majukumu mazito huku akiwataka wenzake kutokubali kutishwa na yeyote “kwani katu hatuwezi kupitisha mswada wowote bila kuufanyia marekebisho.”

“Ikiwa siku yangu itafika, nitakubali yatakayonipata. Lakini sitasaliti nafsi yangu na mapenzi ya moyo wangu kwa sababu hivyo ndivyo nililelewa; katu sitafanya hivyo,” akaeleza.

Bw Orengo aliwakejeli watu aliodai wanajaribu kuzima sauti za wale wasiokubaliana na misimamo yao, akisema wanasiasa kama hao wanarejesha taifa hilo katika “enzi ya giza”.Lakini licha ya kupiga domo kiwango hicho, mnamo Jumanne Orengo alikuwa miongoni mwa maseneta 52 waliopitisha mswada wa BBI huku akiwakwepa wenzake 12 walioupinga wakidai umesheheni kasoro kadha.

“Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya watu wa Siaya, mimi James Orengo napiga kura ya NDIO kwa mswada huu utakaofungua ukusara mpya wa uongozi nchini,” akasema Alhamisi alasiri.

Nao maseneta; Enock Wambua (Kitui), Moses Wetang’ula (Bungoma), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Margaret Kamar (Uasin Gishu), miongoni mwa wengine wa mrengo wa handisheki waliotaka mswada huo ufanyiwe marekebisho, “walikunja mikia” na kuunga mkono ulivyo.

“Baada ya kushauriana kwa kina na kiongozi wa chama changu cha Wiper, Mheshimiwa Kalonzo Musyoka na kwa niaba ya chama hicho na muungano wa Sacred Alliance ninapiga kura ya NDIO,” akasema Bw Wambua, ambaye ni mmoja wa maseneta waliokuwa wamewasilisha maombi kwa afisi ya Spika Kenneth Lusaka wakitaka mswada huo ufanyiwe marekebisho.

Licha ya maseneta wengi wa mrengo wa Tangatanga kupinga mswada huo, baadhi yao walikwenda kinyume na msimamo huu na kupiga kura ya NDIO. Wao ni pamoja na; Seneta wa Mandera Mohamed Maalim Mohamud, John Kinyua (Laikipia), Ledama Ole Kina (Narok), Philip Mpaayei (Kajiado) na Seneta Maalum Alice Milgo.

Msimamo kama huo wa kuyumba pia ulishuhudiwa wiki jana katika kambi hiyo ya Dkt Ruto ambapo wabunge walioapa kufelisha mswada huo waliupitisha wakitoa mseto wa sababu.

Wakiongozwa na Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, baadhi ya wandani hao wa Naibu Rais William Ruto, walidai waliamua kuunga mkono mswada wa BBI kwa sababu umependekeza nyongeza za maeneo bunge katika kaunti zao.

You can share this post!

Atletico Madrid wapepeta Real Sociedad na kunusia taji la...

Buffon aweka rekodi ya kuwa kipa mkongwe zaidi kuokoa...