• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Lempurkel akana shtaka la kueneza chuki Laikipia

Lempurkel akana shtaka la kueneza chuki Laikipia

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Mbunge wa Laikipia kaskazini Bw Mathew Lempurkel alishtakiwa Alhamisi kwa matamshi ya kuchochea uhasama wa kikabila.

Bw Lempurkel aliyeachiliwa kwa dhamana ya Sh150,000 pesa tasilimu alikanusha shtaka la kuchochea uhasama.Shtaka lilisema kati ya Julai 11 na Julai 17 wakati wa mahojiano kwenye kituo cha Televisheni cha Maa Community alidai mashamba ya watu binafsi na hifadhi za wanyama ni mali ya jamii inayozugumza lugha ya Kimaasai almaarufu Jamii ya Maa.

Alidaiwa pia alisema wawekezaji wamiliki mchanga lakini nyasi ni ya Wamaasai.Shtaka lilisema alitaja Jamii ya Kikuyu ile nyayo zao ziko na funza jambo lililopelekea hisia za uhasama kuibuka.

Upande wa mashtaka ulieleza hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Sinkiyian Tobiko kwamba kutokana na matamshi hayo ya kuchochea hisia za chuki ya Bw Lempurkel vurugu zimezuka katika kaunti ya Laikipia ambapo watu kadhaa wameuawa, mifugo kuibwa, uvamizi wa mashamba ya kibinafsi na watu kuhama makwao.

Hata hivyo kiongozi wa mashtaka Bw Abel Omariba alieleza korti hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.Mawakili Thomas Kajwang , Harun Ndubi na Saitabau ole Kanchory walipinga matamshi ya upande wa mashtaka na kusema suala la mashamba katika eneo la Laikipia ni miongoni mwa dhuluma kihistoria zinazopasa kujadiliwa na pande zote kwa njia ya amani ili kupata suluhu.

Wakili Saitabao ole Kanchory (kulia) azugumza na Lempurkel katika mahakama ya Milimani…Picha/RICHARD MUNGUTI

Bw Kanchory alisema shtaka dhidi ya mshtakiwa halina mwelekeo na kamwe halina mashiko kisheria.“Suala la umiliki wa mashamba ambalo lilizugumziwa na Bw Lempurkel wakati wa mahojiano katika kituo cha Televisheni cha Maa ni mojawapo ya dhuluma za kihistoria linalopasa kujadiliwa pasi kuhatarisha haki za wakazi wa maeneo husika,” alisema Bw Kajwang.

Mabw Kanchory na Ndubi walisema adhabu ya shtaka dhidi ya Lempurkeli ni faini isiyozidi Sh1milioni ama kifungo kisichozidi miaka mitatu gerezani.Waliomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

Katika uamuzi wake, Bi Tobiko alisema kesi inayomkabili mshtakiwa iko na umuhimu kwa umma.Kesi hiyo itatajwa Septemba 22, 2021 kwa maagizo

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ya kuondoa harufu mbaya kwenye jokofu

35 kupigania fursa ya kucheza dhidi ya Bandari FC