• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Linturi apigwa breki na Zambia kwa uagizaji mahindi  

Linturi apigwa breki na Zambia kwa uagizaji mahindi  

Na LUKA ANAMI

SERIKALI ya Kenya imepata pigo baada ya Zambia kutangaza kuwa ina uhaba wa mahindi.

Hili limejiri wiki chache baada ya Waziri wa Kilimo nchini, Bw Mithika Linturi na mwenzake wa Zambia, Mtolo Phiri, kutia saini mkataba wa kuruhusu upandaji wa mahindi nchini Zambia kwa mauzo ya nje.

Kulingana na tangazo lililotolewa na Waziri wa Fedha nchini Zambia, Dkt Situmbeko Musokotwane, serikali ya nchi hiyo ina uhaba wa mahindi kutokana na upungufu wa uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Musokotwane alithibitisha habari hizo akisema kuwa nchi hiyo, italazimika kuagiza mahindi nje ya nchi kama njia ya kusuluhisha uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.

Kulingana na waziri huyo, nchi hiyo inakabiliwa na uhaba wa mahindi kutokana na mavuno duni msimu uliopita.

Wiki chache zilizopita, Waziri Linturi, alitangaza kuwa nchi inapanga kuwapa wakulima wa Zambia kandarasi ya kulima na kuleta mahindi nchini.

“Nadhani sote tunafahamu kuwa kumekuwa na uhaba wa mahindi hasa katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania, Congo na Malawi. Serikali iliamua kuruhusu uagizaji wa bidhaa hiyo ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu,” akasema Musokotwane.

“Kadhalika, Hazina ya nchi imeondoa kodi na ada nyingine zinazotozwa bidhaa hiyo kutoka nje ili kusaidia katika kudhibiti gharama za bidhaa hii. Ushuru umeondolewa, sekta binafsi iko huru kuagiza kutoka Afrika Kusini au kutoka popote ili upungufu huo uweze kushughulikiwa,” akaongeza waziri huyo.

Wafanyakazi wakipima na kukausha mahindi kando ya barabara mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru mapema mwaka huu. PICHA / MAKTABA

Kulingana na ripoti ya masuala ya chakula toshelevu ya Julai 2022 hadi Machi 2023, katika suala la uzalishaji wa bidhaa za kilimo, uzalishaji wa mahindi nchini Zambia mwaka wa 2022/2023, ulipungua kutoka tani 3,620,244 msimu uliopita hadi tani 2,706,243 na hivyo kusababisha uamuzi wa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, Musokotwane alisema, hajapokea taarifa kamili kutoka kwa waziri Linturi wala kwa Waziri mwenzake wa Kilimo Mtolo Phiri.

“Hizo ni taarifa ambazo waziri wa Kilimo nchini Zambia anaweza kushughulikia,” akasema Musokotwane.

Licha ya hali hiyo, Zambia imetenga kati ya hekari 20,000 hadi 40,000 kwa ajili ya kukuza zao hilo kwa soko la Kenya.

Hata hivyo, hatua ya Bw Linturi kuagiza mahindi kutoka Zambia kufikia Agosti ilikosolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Wakulima Kenya, Bw Kipkorir Menjo ambaye anasema kuwa uamuzi huo haukufaa.

“Linturi alitangaza kuagiza mahindi kutoka Zambia mwezi wa Agosti 2023, ambao utakuwa wakati wa kuvuna katika maeneo mengi ya Magharibi na Bonde la Ufa na hata Uganda na Tanzania,” akasema Bw Menjo.

Bei ya unga wa mahindi imepanda nchini huku pakiti ya kilo mbili sasa ikiuzwa kwa zaidi ya Sh200 kutoka Sh186 kwa kiasi sawa mwezi uliopita.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Kilimo, Harsama Kello ambaye aliandamana na Bw Linturi nchini Zambia, alisema Kenya inatazamia kuagiza tani milioni moja za mahindi ili kusaidia katika kupambana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

  • Tags

You can share this post!

Inter Milan guu moja ndani ya nusu-fainali za UEFA baada ya...

Man-City yafunza Bayern Munich kusakata soka

T L