• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Man-City yafunza Bayern Munich kusakata soka

Man-City yafunza Bayern Munich kusakata soka

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walijiweka pazuri kufuzu kwa nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kupokeza majabali Bayern Munich kichapo cha 3-0 katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali mnamo Jumanne usiku ugani Etihad.

Erling Haaland alifunga bao la tatu la Man-City katika dakika ya 76 na kufikisha jumla ya magoli 45 msimu huu. Ufanisi huo unamfanya kuwa mchezaji anayejivunia mabao mengi zaidi kwenye mashindano yote katika msimu mmoja tangu kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kianzishwe miaka 30 iliyopita. Nyota huyo raia wa Norway sasa amevunja rekodi za ufungaji mabao za Mohamed Salah na Ruud van Nistelrooy.

Huku Man-City sasa wakiwa pua na mdomo na kutinga hatua ya nne-bora ya UEFA msimu huu, Bayern ya kocha Thomas Tuchel ina kibarua kizito itakapokuwa mwenyeji wa masogora wa kocha Pep Guardiola kwenye marudiano ugani Allianz Arena.

Rodri alifungulia Man-City ukurasa wa mabao katika dakika ya 27 kabla ya Bernardo Silva kufunga bao la pili la baada ya kushirikiana vilivyo na Haaland kunako dakika ya 70.

Zaidi ya kufukuzia kombe la UEFA msimu huu, miamba hao wawili wapo pazuri kuhifadhi ubingwa wa ligi zao za nyumbani.

Sawa na Bayern waliotandika SC Freiburg 1-0 katika pambano lao lililopita ligini, Man-City nao walishuka dimbani wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 4-1 dhidi ya Southampton 4-1 wikendi iliyopita ugani St Mary’s.

Ushindi huo ulikuwa wa nane mfululizo kwa Man-City kusajili na uliweka hai matumaini yao ya kumaliza kampeni za msimu huu na mataji matatu – Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na UEFA.

Masogora hao wa Guardiola sasa wamepachika wavuni mabao 34 kutokana na michuano tisa iliyopita. Wanajivunia alama 67 kutokana na mechi 29 za EPL na watatawazwa wafalme wa kipute hicho iwapo watashinda mechi zote tisa walizosalia nazo ligini muhula huu wa 2022-23.

Haaland amekuwa mhimili muhimu wa Man-City msimu huu na anatarajiwa kuwa tegemeo kubwa dhidi ya Bayern katika pambano la mkondo wa pili. Mvamizi huyo wa zamani wa RB Salzburg na Borussia Dortmund amepachika wavuni mabao 30 katika EPL msimu huu na amecheka na nyavu za wapinzani mara 11 kutokana na michuano saba iliyopita ya UEFA.

Alifunga magoli matano katika ushindi wa 7-0 dhidi ya RB Leipzig na akasaidia Man-City kudengua kikosi hicho cha Ujerumani kwa jumla ya mabao 8-1 katika hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Mechi ya Jumanne ilikuwa ya kwanza kati ya nane kwa Haaland kutamba dhidi ya Bayern huku akipoteza mechi zote saba za awali dhidi ya kikosi hicho alipokuwa akivalia jezi za Dortmund.

Man-City waliwahi kukutana na Bayern katika miaka yao ya mwanzo katika soka ya bara Ulaya na wakashinda mechi mbili kati ya tatu ugani Etihad. Kichapo cha pekee walichopokezwa na Bayern nyumbani ni cha 1-0 katika hatua ya makundi ya UEFA mnamo Septemba 2014 Guardiola akidhibiti mikoba ya miamba hao wa Ujerumani.

Licha ya kudhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern wamekuwa wakisajili matokeo mseto kwenye kivumbi hicho na sasa wana presha zaidi ya kudumisha ubabe wao chini ya kocha mpya, Tuchel.

Mtangulizi wa Tuchel, Julian Nagelsmann, aliongoza Bayern kuhimili ushindani mkali katika Kundi C lililojumuisha Inter Milan, Paris Saint-Germain (PSG) na Viktoria Plzen.

Katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Bayern, Tuchel aliongoza waajiri wake kupepeta Dortmund ligini ugani Allianz Arena. Hata hivyo, masogora wake waling’olewa na Freiburg kwenye robo-fainali ya DFB-Pokal (German Cup) kwa mabao 2-1 siku chache baadaye.

Japo Bayern walilipiza kisasi dhidi ya Freiburg wikendi iliyopita, miamba hao wamekamilisha mechi sita pekee kati ya 17 zilizopita bila kufungwa bao na wameokota mpira kimiani angalau mara mbili au zaidi katika michuano sita kati ya hiyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Linturi apigwa breki na Zambia kwa uagizaji mahindi  

Drama landilodi akifunga kanisa kwa kutolipwa kodi

T L