• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Maafisa wa NIS washtakiwa kunyang’anya mfanyabiashara dola za Kimarekani 160,000

Maafisa wa NIS washtakiwa kunyang’anya mfanyabiashara dola za Kimarekani 160,000

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watatu wa polisi kutoka kitengo cha Ujasusi (NIS) wameshtakiwa kumnyang’anya kimabavu mfanyabiashara Dola za Kimarekani (USD-$) 160,000 (KSh23,360,000).

Watatu hao Charles Gichohi Muchoya, Cyprian Njagi Ironcho na Roy Opiyo Odunga walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi, Bi Wandia Nyamu.

Walishtakiwa kumnyang’anya Said Omar Mohammed pesa hizo katika eneo la Westlands Nairobi.

Muchoya, Ironcho na Odunga walikana mashtaka yaliyosema kwamba mnamo Juni 22,2023 wakiwa wamejihami na mabastola walimnyang’anya Said Omar Mohammed $160,000 (KSh23,360,000).

Kiongozi wa mashtaka aliambia mahakama watatu hao walimtishia maisha Mohammed wakati wa utekelezaji wa uhalifu huo.

Pia hakimu alifahamishwa watatu hao walishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani.

Muchoya, Ironcho na Odunga waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakiahidi kwamba “hawatatoroka ila watafika kortini kila wanapotakiwa kujibu kesi.”

Upande wa mashtaka haukupinga ombi la maafisa hao wa polisi kitengo cha ujasusi (NIS) kuachiliwa kwa dhamana.

Bi Nyamu aliwaachilia maafisa hao kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu kila mmoja ama dhamana ya Sh300,000  kila mmoja.

Hakimu aliagiza washtakiwa wapewe nakala za ushahidi waandae tetezi zao.

Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Septemba 23 kutengewa siku ya kusikizwa.

  • Tags

You can share this post!

Shule zalia shida Serikali ikikosa kuzitumia pesa

Huyu anataka tupime ilhali niliokuwa nao walichovya bila...

T L