• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Shule zalia shida Serikali ikikosa kuzitumia pesa

Shule zalia shida Serikali ikikosa kuzitumia pesa

Na DAVID MUCHUNGUH

WIKI tatu baada ya shule kufunguliwa kwa muhula wa tatu, Wizara ya Elimu bado haijatuma pesa kwa shule za umma.

Kutokana na hilo, baadhi ya shule zimeanza kuwatuma wanafunzi nyumbani kwa kutolipa karo huku wengine wakitarajiwa kufukuzwa shuleni wiki ijayo. Serikali humlipia kila mwanafunzi wa sekondari Sh22, 244, yule wa shule za msingi Sh1,420 na Sh15,042 kwa anayesomea sekondari ya msingi.

Usimamizi wa shule mbalimbali na miungano ya walimu, imeomba serikali itoe pesa hizo ambazo ni za kudhamini masomo bila malipo katika shule za msingi na upili. Wanasema kutotumwa kwa pesa hizo kumechangia matatizo katika uendeshaji wa shughuli za shule.

“Wakati mwingine huwa hatuna jingine ila kuwatuma wanafunzi nyumbani. Tatizo ni kuwa sasa hata wazazi wenyewe hawatumi pesa ilhali tunahitaji kuendesha shughuli za shule,” akasema Mwalimu Mkuu mmoja kutoka Kaunti ya Meru.

“Huu ni muhula wa tatu na sasa tupo njiapanda kuamua iwapo tutamakinikia kuwanoa wanafunzi ili wapate matokeo mazuri au kusaka pesa za kuwaweka shuleni. Huwa tunajaribu sana kujiepusha kuwatuma wanafunzi nyumbani,” akaongeza.

Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Nchini, Bw Johnson Nzioka, alisema kusambazwa kwa fedha hizo kumekuwa kukifanyika kwa kuchelewa na sasa shule zinaandamwa na madeni ya mamilioni ya pesa.

“Kuendesha shughuli za shule sasa ni ngumu. Kibarua kikubwa kitatokea wakati wa kununua vifaa vya mitihani kwa kuwa hakuna pesa na pia kuna mahitaji mengine kama mishahara ya wafanyakazi,” akasema Bw Nzioka kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Mwenyekiti huyo alisema pesa ambazo walipata kwenye muhula wa pili hazikutosha na zilielekezwa katika kupunguza madeni.

Mwalimu Mkuu mwengine alisema hatua ya pesa kuchelewa kutumwa kutaathiri maandalizi ya mitihani ya utendaji kwa sababu vifaa na kemikali zinazohitajika hazitakuwa zimenunuliwa. Mitihani ya Kitaifa inatarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.

“Ingawa bado hatujapata maelezo ya vifaa vinavyohitajika kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), tunajua kuwa ni bei ghali hasa kipindi hiki cha mtihani. Shule zinaandamwa na madeni na ni aibu sana bado kuwaendea wawasilishaji bidhaa wanaokudai,” akasema.

Mwenyekiti wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili Nchini (KESSHA), Bw Indimuli Kahi, jana aliitaka serikali iharakishe kutuma pesa hizo jinsi tu ilivyotoa pesa ambazo zilikuwa zikidaiwa na kaunti.

“Shule za kutwaa ambazo zinategemea hela hizo kuendesha shughuli zao za kila siku ndizo zimeathirika sana. Wawasilishaji bidhaa wanasisitiza kuwa lazima walipwe madeni yao mwanzoni na pia muhula huu shule zinastahili kununua karatasi za kudurusu kwa wanafunzi wakijiandaa kwa mitihani ya kitaifa,” akasema Bw Indimuli.

Wakati wa Kongamano la Walimu Wakuu mnamo Juni katika jiji la Mombasa, Bw Kahi alisema kuwa kila mwanafunzi katika shule za sekondari anastahili kulipiwa deni la Sh8,901 japo Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alikanusha takwimu hiyo.

  • Tags

You can share this post!

‘Ex’ wa Diamond Platnumz, Hamisa Mobetto akana...

Maafisa wa NIS washtakiwa kunyang’anya mfanyabiashara...

T L