• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Maafisa wa zamani KEMSA wakiri kuikosesha Kenya Sh74 milioni

Maafisa wa zamani KEMSA wakiri kuikosesha Kenya Sh74 milioni

NA MARY WANGARI

USIMAMIZI wa awali wa Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Matibabu Nchini (KEMSA) umekiri kwamba ulivuruga kandarasi yake na Hazina ya Kimataifa hatua iliyoisababishia Kenya hasara ya mamilioni.

Kenya ilipoteza Sh74 milioni baada ya Hazina ya Kimataifa kukatiza mkataba wake na Kemsa kuhusu ununuzi wa vyandarua vya kujikinga na malaria na kupatia kandarasi hiyo shirika la Wambo.org, Seneti ilielezwa katika kikao Jumanne.

Kupitia nakala zilizowasilishwa mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago, Kemsa ilikiri kuwa Kenya ilipoteza fursa ya kupata asilimia mbili ya thamani ya mchakato huo kiasi cha Sh3.7 bilioni.

Akijibu maswali mbele ya Seneti, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kemsa, John Kabuchi, alionekana kukubaliana na masuala yaliyotajwa na Hazina ya Kimataifa yaliyosababisha kandarasi hiyo kufutiliwa mbali.

“Ni kweli kwamba tunahitaji kutathmini upya michakato yetu,” Bw Kabochi alieleza Seneti.

Hazina ya Kimataifa kupitia mwakilishi wake nchini, kampuni ya PriceWaterhouseCoopers, ilitaja masuala kadhaa kama yaliyochangia kukatiza mkataba wake na KEMSA.

Baadhi ya masuala yaliyotajwa ni pamoja na misukosuko ya uongozi ambapo kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kwa wakurugenzi, maafisa wakuu wa usimamizi na wanachama wa Bodi ya KEMSA.

“Mchakato wenyewe wa ununuzi ni kitendawili kigumu, mrefu na aghalabu huchelewa. Uchunguzi ulionyesha kuwa kuchukua muda mwingi na ucheleweshaji bado ni udhaifu mkuu katika mchakato wa ununuzi, hata katika mfumo wenye vipimo,” ilisema nakala iliyowasilishwa na PWC kwa Seneti.

Suala la ushuru wa forodha na ada nyinginezo za ushuru unaotozwa ununuzi wa Hazina ya Kimataifa vilevile lilitajwa kama kizingiti.

Hata hivyo, shirika hilo la kimataifa la kutoa ufadhili lilisema kuwa halijapoteza imani na Kemsa kuhusiana na ununuzi wa matibabu muhimu ya HIV, Kifua kikuu na malaria.

Aidha, lilirejelea  mwanzoni mwa mpango huo wa kutoa ufadhili ambapo Kemsa iliwezesha kukoa mamiloni ya pesa na kununua kiasi maradufu cha dawa za ARV.

“Bei bora za Kemsa ziliwezesha kuokoa zaidi ya Sh1.4 milioni katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango huu hali iliyowezesha ununuzi wa kiasi zaidi cha ARV katika mwaka wa pili,” alisema Mkurugenzi wa PWC, Francis Muriu.

“Kwa mfano, pesa hizo kupitia Kemsa zimewezesha Hazina ya Kimataifa kuongeza maradufu idadi ya pakiti za dawa aina ya TLD-90 katika mwaka wa pili na kusambaza pakiti milioni tatu badala ya kiasi asilia kilichopangiwa cha pakiti 1.5 milioni,” alisema Bw Muriu.

Kulingana na Bw Muriu, “Pesa zilizookolewa ziliweza kukidhi mahitaji ya wagonjwa wote watu wazima wanaougua HIV kwa kuhakikisha wanapata TLD-90 kwa miezi saba. Tumeokoa raslimali vilevile katika ununuzi wa dawa za kutibu malaria na kifua kikuu.”

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yawazuia maafisa kumkamata Aladwa

Mabunge ya Kenya na Australia kushirikiana kiutendakazi

T L