• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Magavana Pwani walalamikia uhaba wa walimu wakisema unachangia matokeo duni ya mitihani  

Magavana Pwani walalamikia uhaba wa walimu wakisema unachangia matokeo duni ya mitihani  

WINNIE ATIENO na MKAMBURI MWAWASI

GAVANA wa Kilifi Gideon Mung’aro na mwenzake wa Taita Taveta Andrew Mwadime wameitaka Serikali ya Kitaifa kushughulikia uhaba wa walimu katika eneo la Pwani.

Magavana hao walisema ukosefu wa walimu wa kutosha umechangia kupungua kwa viwango vya elimu katika eneo hilo.

“Tunashughulikia changamoto ya matokeo duni ya mitihani ya kitaifa, ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na uhaba wa walimu katika shule zetu,” alisema Gavana Mung’aro kwenye maombi maalum katika Uwanja wa Shule ya upili ya Malindi High.

Alisema viongozi wa Pwani watatetea kuajiriwa kwa walimu katika nafasi za kazi zilizotangazwa hivi majuzi na Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) ili kuziba pengo lililoko.

Ili kukuza na kuinua viwango vya elimu, Bw Mung’aro alisema utawala wake unapiga msasa Mswada wa Hazina ya Elimu ya Wadi 2018, ili kuongeza mgao wa hazina hiyo kutoka Sh350 milioni hadi Sh500 milioni.

“Nyongeza hii inalenga kusaidia wanafunzi wengi zaidi kupata elimu bora,” alisema Gavana Mung’aro.

Haya yanajiri wiki chache baada ya viongozi wa kisiasa Pwani kufanya kikao na Rais William Ruto kujadili kudorora kwa viwango vya elimu eneo hilo.

Rais Ruto alikiri kuwa kuna changamoto katika sekta ya elimu eneo la Pwani akiahidi kushirikiana na uongozi wa Pwani kutatua kero hiyo.

Rais Ruto alisema uongozi wake ulitoa nafasi za kuajiri walimu 5,000 kutoka eneo la Pwani.

Hata hivyo, bado walimu wa Pwani hawajajaza idadi hiyo kutokana na uhaba wa walimu.

“Kuna pengo la walimu 350 na bado kuna nafasi za walimu. Viongozi wa Pwani wanafaa kuhakikisha wanafunzi wanachukua nafasi za ualimu katika Taasisi za mafunzo ya Ualimu vilivyoko eneo ili kupata nafasi za kazi serikalini,” alisema Rais Ruto.

Naye Gavana Mwadime ameitaka TSC kutilia maanani kilio cha walimu kote nchini akiongeza kuwa serikali imechukua muda mrefu kutatua uhaba wa walimu unaoshuhudiwa nchini hasa ukanda wa Pwani.

Alisema baadhi ya shule zina idadi kubwa ya wanafunzi huku zikikabiliana na uhaba wa walimu.

“Licha ya changamoto wanazopitia ikiwemo baadhi ya maeneo wanayohudumu kutojumuishwa kama maeneo yenye changamoto katika utoaji wa huduma walimu bado wamejitolea kuhakikisha wanaboresha viwango vya elimu,” alisema.

Akiongea kwenye mkutano na Muungano wa Walimu wa chama cha KUPPET tawi la kaunti hiyo mjini Wundanyi, Bw Mwadime aliahidi kushirikiana na wabunge kuhakikisha suluhu ya baadhi ya changamoto hizo inapatikana.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali za Kaunti zatakiwa kuajiri wahudumu zaidi wa afya

Kenya Power yamulikwa kwa madai ya kuitisha hongo ya Sh200,...

T L