• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kenya Power yamulikwa kwa madai ya kuitisha hongo ya Sh200, 000 kurejesha stima

Kenya Power yamulikwa kwa madai ya kuitisha hongo ya Sh200, 000 kurejesha stima

NA SAMMY WAWERU

KAMPUNI ya Usambazaji Nguvu za Umeme Nchini, ndiyo Kenya Power kwa mara nyingine imemulikwa kufuatia tetesi baadhi ya maafisa wake wanaitisha hongo kurejesha stima katika mtaa mmoja Nairobi.

Wakazi wa Carwash, Zimmerman, eneo lililoathirika baada ya nguvu za umeme kupotea wiki moja iliyopita wanalalamikia kukaa kwenye giza huku kampuni hiyo ikisemekana kuitisha mlungula ili kutatua changamoto hiyo.

Sehemu ya mtaa huo imesalia bila stima tangu Jumatano, Novemba 8, 2023 jioni.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa Kenya Power maafisa walioarifiwa kuhusu hitilafu ya transfoma iliyosababisha Carwash kusalia bila nguvu za umeme kufikia sasa wanaagiza hongo ya shilingi laki mbili.

“Walipofahamishwa kuhusu hali ilivyo, waliweka sharti la hongo ya Sh200, 000 ili warejeshe stima,” akaarifu mfanyabiashara anayehudumu mtaani humo, na ambaye tutabana majina yake kwa sababu za kiusalama.

Akikadiria hasara kubwa ya uharibifu wa bidhaa za kula anazouza, analalamikia utepetevu wa Kenya Power.

Eneo la Carwash limekuwa likishuhudia changamoto za stima kupotea, transfoma inayosambaza moto humo ikitajwa kuwa kitega uchumi cha maafisa wenye tamaa wa Kenya Power.

“Si mara ya kwanza transfoma ya mtaa huu kuwa na tatizo kisha Kenya Power inaitisha hongo kuishughulikia. Mei 2023, ilikuwa na hitilafu na mahesabu yakikokotolewa walikabidhiwa kitita kinachokaribia Sh1 milioni kurejesha umeme,” mjuzi wetu akaarifu.

Transfoma mtaa wa Carwash, Zimmerman, Kaunti ya Nairobi ambayo wakazi wanalalamikia kutumika na baadhi ya maafisa Kenya Power kuitisha hongo. PICHA|SAMMY WAWERU

Novemba 8, 2023, wafanyakazi wa Kenya Power wanasemekana kuondoa fiusi zinazosambaza moto kwa majengo na makazi yaliyoathirika kwa madai kuna aliyecheza na transfoma husika.

“Walitoa fiusi kwa hasira na wakati wa tukio walikuwa na transfoma nyingine waliyopaswa kubadilisha,” akafichua mmoja wa malandilodi Zimmerman, akishangazwa na tabia za Kenya Power.

“Ikiwa kuna mtu aliyejaribu kuhitilafiana na transfoma yenyewe, kwa nini mhusika asichukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria?” mmiliki huyo wa ploti akataka kujua.

Cha kushangaza ni kwamba Kituo cha Polisi Zimmerman kipo mita chache kutoka kwa transfoma inayotajwa kuwa tatizo, jambo linaloibua maswali kuhusu utendakazi wa kampuni hiyo.

Aidha, Taifa Leo Dijitali ilipowasiliana na kampuni hiyo mnamo Novemba 11, 2023 kwa njia ya simu, wenyeji walishauriwa kutafutana na ‘wakubwa wa Kenya Power kupata transfoma nyingine’.

“Ni jukumu lao kufikia wakubwa kwa sababu hatua za kupata transfoma ni ndefu,” akasema mmoja wa wahudumu aliyetumia nambari za simu: 0711031000 kujibu malalamishi, ambazo ni kati ya zinatumika kuwasiliana na wateja.

Alikiri kupokea malalamiko ya raia kuhusu transfoma eneo hilo.

Nyumba za kupangisha Carwash, zinahudumu chini ya Zimmerman Settlement Scheme.

Mtaa huo unapakana na Thika Super Highway, barabara maarufu inayounganisha jiji la Nairobi na mji wa Thika.

Eneo lililoathirika na kupotea kwa nguvu za umeme li kilomita chache kutoka kituo cha Kenya Power cha Roysambu.

Licha ya malalamishi ya wenyeji, tetesi zinahoji kuna baadhi ya majengo yaliyounganishwa umeme kwa njia haramu.

Ni jukumu la Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kwa ushirikiana na Idara ya Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI), kufanya uchunguzi wa kina Carwash ikizingatiwa kuwa Kenya Power ni shirika la kiserikali ambalo halipaswi kutoza ada yoyote kurejesha umeme unapopotea au kurekebisha tatizo.

  • Tags

You can share this post!

Magavana Pwani walalamikia uhaba wa walimu wakisema...

Waziri wa Afya asihi wakazi wakuze miti kwa matumizi ya dawa

T L