• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Magavana wageuka kuwa ‘miungu’ badala kuwa watumishi

Magavana wageuka kuwa ‘miungu’ badala kuwa watumishi

NA JUSTUS OCHIENG

IWAPO ugatuzi ulitarajia kuwepo kwa magavana watumishi wanaofanya kazi na wananchi vijijini na kuwasaidia kuamua miradi inayoweza kutekelezwa, basi, kwa msingi huo pekee, umekosa kutimiza malengo yake.

Hii ni kwa sababu magavana wamekuwa wakijichukulia kama ‘marais wadogo’, wanaoonyesha utajiri kupitia viti vya mamilioni ya pesa, ving’ora na magari ya kifahari na viongozi wanaotoa maagizo badala ya kuwa watumishi wa raia.

Lakini mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bi Anne Waiguru anapinga haraka taswira hii, akisema matokeo chanya muhimu yamepatikana kupitia ugatuzi.

“Kwa upande wa mafanikio kote nchini, huduma muhimu, hasa afya, elimu ya chekechea, kilimo na barabara za vijijini zimeimarika tangu ugatuzi ulipoanzishwa mwaka 2013. Miji mingi ya vijijini pia imeboreshwa,” asema Bi Waiguru, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa kwanza wa Ugatuzi nchini.

Hivi majuzi, mipango ya madiwani wa kaunti ya Kakamega kuanzisha afisi ya mke wa gavana ilizua hasira.

Wakosoaji wa Mswada wa Afisi ya Mke wa Gavana wa Kakamega wa 2023, walishikilia kuwa ukitekelezwa, unaweza kuigwa katika kaunti 47 na kufanya kaunti kupoteza mamilioni ya pesa zinazoweza kutumika kuboresha maisha ya raia.

Baada tu ya mwaka mmoja ofisini mnamo 2013, magavana waanzilishi walianza kwa mwelekeo mbaya, na kuzua utata kwa azma yao ya kupeperusha bendera za kitaifa kwenye magari yao, hatua ambayo hata hivyo ilikatizwa na Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale ambaye alifadhili Mswada uliolenga kuwakataza wakuu hao kupeperusha bendera ya taifa na kutumia jina la “Mtukufu.”

Rais Uhuru Kenyatta alitia saini Mswada huo kuwa Sheria 2014, ambapo alipiga marufuku magavana kupeperusha bendera kwenye magari yao.

Jaji Isaack Lenaola, hata hivyo, alibainisha kuwa Magavana wanaweza kupeperusha bendera za kaunti.

Hata hivyo, magavana hao, hadi sasa wameendelea kutambuliwa kwa jina la heshima “Mstahiki” ambalo kwa kawaida huhifadhiwa kwa ajili ya rais.

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALA) James Mwamu anasema magavana walilazimika kuzuiwa kupeperusha bendera ya taifa “kwa kuwa ni mali ya Serikali ya Kitaifa inayoakisi utambulisho wa kitaifa wa Jamhuri ya Kenya na wala si wa kaunti yoyote ndani ya Kenya.”

Bw Mwamu anasema Katiba imeipa Serikali ya Kitaifa mamlaka ya kikatiba ya kusimamia matumizi ya bendera ya taifa.

“Pia ilijadiliwa na Bunge la Kitaifa kwamba kupeperusha bendera kwenye gari si mojawapo ya kazi zilizogatuliwa ndani ya malengo ya huduma za ugatuzi kutoka Serikali ya Kitaifa hadi ya Kaunti,” asema.

Prof Gutile Naituli anasema tamaa zisizo za kisheria za magavana zilihitaji kuzuiliwa.

Aidha, anakumbuka kwamba, magavana walikuwa wakishinikiza wachukuliwe kama ‘marais’ wa kaunti na kupewa kinga dhidi ya kushtakiwa sawa na kinga ya rais chini ya Kifungu cha 143 cha Katiba.

Ilihitajika kufafanuliwa kwamba Baraza la Magavana (COG) si kikundi cha kushawishi au chama cha wafanyakazi kushinikiza ustawi wa magavana au kuwakinga dhidi ya uwajibikaji.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala kutia mfukoni Sh850,000 licha ya kushika nafasi ya...

Wezi wanaolenga maduka ya bidhaa za kula na za matumizi...

T L