• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:57 PM
Magavana waliovuta ?mkia sasa wajitetea

Magavana waliovuta ?mkia sasa wajitetea

Na WAANDISHI WETU

BAADHI ya magavana ambao waliorodheshwa nyuma katika utafiti wa utendakazi, wamejitetea vikali.

Gavana wa Taita Taveta, Bw Granton Samboja alisema shirika la utafiti la Infotrak halikuzingatia changamoto zilizokumba kaunti hiyo kwa muda mrefu mwaka uliopita.

Kulingana naye, mvutano uliokuwepo miongoni mwa afisi yake na madiwani uliathiri sana utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi alidai kwamba shirika hilo lilitaka atoe pesa ili aorodheshwe katika nafasi bora.

“Hatuwezi kutikiswa na orodha hiyo. Walikuja katika afisi yangu wakitaka pesa ili niwekwe katika nambari moja lakini nikakataa,” akadai Bw Murungi.

Kupitia kwa taarifa, Gavana Samboja alisema kati ya Juni na Desemba mwaka uliopita, utawala wake ulikumbwa na mvutano tele na madiwani kuhusu bajeti hadi uamuzi ukafanywa ang’olewe mamlakani.

Utafiti wa Infotrak ulifanywa kati ya Oktoba na Desemba mwaka uliopita.

Katika Kaunti ya Isiolo, baadhi ya wakazi walimlaumu Gavana Mohamed Kuti kwa kuzembea kazini baada ya kuorodheshwa katika nafasi ya 39.

Kwingineko Homa Bay, mashirika ya kutetea haki za umma yalimtaka Gavana Cyprian Awiti awafute kazi maafisa wa kaunti ambao wana maazimio ya kuwania nafasi za kisiasa.

Kulingana na viongozi wa mashirika hayo, maafisa hao ndio wamelegea kazini kwani wanatumia muda mwingi kutafuta umaarufu wa kisiasa badala ya kutumikia umma.

Kaunti ya Homa Bay ndiyo ilivuta mkia kati ya kaunti zote za Nyanza.

Inaaminika idadi kubwa ya maafisa wa kaunti wanataka kuwania nyadhifa za kisiasa kwa vile Bw Awiti anatumikia awamu yake ya mwisho na hana nia ya kuwania wadhifa mwingine wa kisiasa ifikapo mwaka wa 2022.

Kwenye orodha hiyo iliyotolewa Jumatano, Wycliffe Oparanya wa Kakamega aliorodheshwa bora zaidi akifuatwa na Salim Mvurya wa Kwale na Kivutha Kibwana wa Makueni.

You can share this post!

BBI: Raila aikosoa IEBC, asema ‘refarenda itagharimu...

Pigo kwa Bunge huku mahakama ikizima sheria 23