• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Magoha asisitiza ni sharti wanafunzi waliojifungua warejee shuleni

Magoha asisitiza ni sharti wanafunzi waliojifungua warejee shuleni

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amesisitiza Ijumaa kwamba wanafunzi wa kike waliopata ujauzito mwaka 2020 ni lazima warejee shuleni kukata kiu ya masomo.

Prof Magoha amesema haijalishi ikiwa wamejifungua au la, ila lazima waendeleze safari ya masomo kuafikia ndoto zo.

Shule zilifunguliwa mnamo Januari 4, 2021, ili kuendelea na kalenda ya masomo ya 2020, miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini.

Likizo hiyo ya lazima, ikizingatiwa kuwa shule zote nchini na taasisi za elimu ya juu zilifungwa Machi 2020, kama njia mojawapo kuzuia maenezi ya virusi hatari vya corona, kipindi ambacho wanafunzi walisalia nyumbani baadhi ya wale wa kike walipachikwa mimba.

“Wale ambao tutaruhusu kukaa nyumbani kwa sasa ni waliosalia na siku chache sana kujifungua, baadaye watarejea shuleni kukata kiu yao ya masomo,” akasisitiza Prof Magoha.

Waziri huyo wa Elimu alisema hayo katika zaira yake kutathmini ufunguzi wa shule eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu.

Shughuli za masomo Nyando zimeathirika kufuatia mafuriko ya mvua eneo hilo, ambayo yamefunika baadhi ya shule.

Wanafunzi wa shule zilizoathirika hata hivyo wamehamishiwa katika shule zingine.

Serikali imesema itawachukulia hatua kali kisheria wahuni wahusika wa mimba za mapema kwa watoto wa shule.

Takwimu za idara ya afya zinaonyesha 2020 idadi ya wasichana wa shule waliotungwa ujauzito ni ya juu mno, ikilinganishwa na miaka ya awali.

Wakati huo huo, Prof Magoha ametoa onyo kwa walimu wakuu wa shule za umma za msingi na walimu, akiwataka kutotuma nyumbani watoto kwa minajili ya ukosefu wa karo.

Alisema serikali ya kitaifa imetoa kima cha Sh4 bilioni kufadhili shughuli za masomo shuleni.

“Ifahamike wazi kuwa masomo nchini ni ya bure, hayatozwi malipo,” akasema Prof Magoha.

Elimu bila malipo kwa shule za msingi za umma ilianza chini ya utawala wa Rais Mstaafu, Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga aliyehudumu kama Waziri Mkuu.

Serikali ya Jubilee, inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto iliendeleza mfumo huo walipochukua hatamu ya uongozi 2013.

You can share this post!

LISHE: Ugali na dagaa

Kenya kuandaa mashindano ya kimataifa ya tenisi kwa...