• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Kenya kuandaa mashindano ya kimataifa ya tenisi kwa chipukizi kuanzia Januari 18

Kenya kuandaa mashindano ya kimataifa ya tenisi kwa chipukizi kuanzia Januari 18

Na CHRIS ADUNGO

KENYA itakuwa mwenyeji wa makala ya kwanza ya mchezo wa kimataifa wa tenisi kwa chipukizi almaarufu Tennis Federation (ITF) World Junior Circuit.

Mashindano hayo yameratibiwa kuandaliwa katika uwanja wa Nairobi Club na yatafanyika kwa kipindi cha wiki nane mwaka huu wa 2021.

Kivumbi hicho kitatandazwa kwa kipindi cha wiki tatu mnamo Januari, wiki mbili katika mwezi wa Julai na majuma matatu mnamo Novemba. Duru ya Januari itafunguliwa rasmi tarehe 18 na kitaendeshwa kwa wiki tatu. Jumla ya mataifa 17 yamethibitisha kunogesha kivumbi hicho, yakiwemo India, Ufaransa, Urusi, Norway na wenyeji Kenya.

Kwa mujibu wa James Kenani ambaye ni Rais wa Shirikisho la Tennis Kenya (TK), mafanikio ya kuandaa kipute hicho cha kimataifa yatawapa jukwaa zuri la kutathmini kiwango cha maendeleo ya mchezo huo humu nchini ikizingatiwa kwamba mashindano mengi ya mwaka 2020 yalifutiliwa mbali kwa sababu ya janga la corona.

“Tuna matumaini ya kuanza mwaka kwa matao ya juu. Ni tija na fahari kwa Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) kutuaminia fursa ya kuwa wenyeji wa mashindano haya ya haiba kubwa,” akasema Kenani kwa kusisitiza kwamba TK itateua kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya kwenye mashindano hayo kutokana na matokeo yaliyoandikishwa na wachezaji mbalimbali katika kampeni za mwaka wa 2020.

TK iliongoza wachezaji wa humu nchini kushiriki mapambano manne pekee msimu uliopita wa 2019-20 yakiwemo yale ya Afrika Mashariki, kufuzu kwa fainali za BNP World Team Cup Africa, Davis Cup Euro/Africa na Tennis Kenya Senior & Junior Challenge.

Mashindano ya kila mwaka ya Kenya Open, Nairobi Open na Karen Open yalifutiliwa mbali kutokana na hofu ya maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Katika kitengo cha ITF World Juniors, wasichana watakaowakilisha Kenya ni Debbie Akoth, Cynthia Wanjala, Shakira Varese, Angela Okutoyi ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya 271 kwenye orodha ITF Junior pamoja na dada yake pacha, Roselida Asumwa. Itakuwa mara ya kwanza kwa Akoth kuvalia jezi za timu ya taifa.

Derick Ominde, Jayson Mbongoro, Kael Shalin Shah, Raymond Oduor, Brandon Sagala na Reesh Haria watakuwa tegemeo la Kenya katika kitengo cha wavulana.

Mara ya mwisho kwa vikosi vya wanatenisi chipukizi wa Kenya kujitosa ulingoni ni Novemba 2020 ambapo TK iliandaa duru za mashindano ya Senior & Junior Challenge baada ya takriban miezi tisa bila pambano lolote.

Duru ya kwanza kati ya nane zilizopangiwa kufanyika mnamo 2020 iliandaliwa kati ya Novemba 23 na Disemba 10 na ilijumuisha idadi kubwa ya wanatenisi wa kike na kiume walionogesha kivumbi hicho ugani Nairobi Club chini ya uzingativu wa kanuni kali za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Reha Kipsang na Faith Urasa waliibuka washindi wa kategoria ya Junior Challenge baada ya kujizolea alama sita kwa kushinda seti tatu kutokana na jumla ya sita zilizochezwa.

Katika kitengo cha wacheza wawili wawili kwa upande wa wavulana, Reesh Haria na Sahil Chana waliwazidi ujanja Benjamin Tekeo na James Kang’ethe kwa seti 6-0 chini ya kipindi cha saa moja.

Kukamilika kwa ITF World Junior Circuit kunatarajiwa kupisha makala ya 10 ya Nairobi International Junior Circuit na makala ya 12 ya Kenya International Junior Circuit kwenye kalenda ya mashindano hayo ya tenisi msimu huu.

You can share this post!

Magoha asisitiza ni sharti wanafunzi waliojifungua warejee...

Joho ataka Raila aunge Mpwani kuwania urais