• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Mahakama: Ni wakati Rais akubali miito

Mahakama: Ni wakati Rais akubali miito

Na MHARIRI

NI wazi imefikia wakati Rais Uhuru Kenyatta atathmini tena msimamo wake kuhusu mvutano uliopo kati ya Serikali na Idara ya Mahakama.

Sababu kuu ni kuwa ilivyo sasa, ni wazi amekosea kuhusu mwelekeo ambao amechukua kuihusu idara hiyo muhimu.Katika hali ya kawaida, huwezi kuwa sahihi wakati kila mtu anapokukosoa kuhusu kitendo, mwelekeo ama mtazamo kuhusu jambo fulani.

Katika tukio kama hilo, lazima mtu aanze kutathmini tena alipokosea kwani wakosoaji wake wote hawawezi kuwa wanamtakia mabaya.Tangu Rais Kenyatta aanze kuonekana kuingilia uhuru wa mahakama miezi kadhaa iliyopita, hakuna aliyedhani mvutano huo ungefikia kiwango tunachoshuhudia kwa sasa.

Hapo jana, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, alijitokeza wazi na kumwambia Rais kwamba amekosea kuhusu mwelekeo aliochukua.Bw Odinga aliungana na watu wengine maarufu kama majaji wastaafu Dkt Willy Mutunga na David Maraga, Jaji Mkuu Martha Koome, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kati ya wengine.

Kwenye taarifa yake jana, Bw Odinga alisema kuwa hakuna tawi lolote la serikali linaloweza kuendesha majukumu yake bila kutegemea jingine.Kauli ya Bw Odinga ni yenye uzito mkubwa ikizingatiwa yeye ni kiongozi mwenye ufuasi wa karibu nusu ya nchi.

Wengi walifasiri kuwa huenda Bw Odinga akalinyamazia suala hilo kutokana na ukaribu alio nao na Rais kutokana na handisheki.Hata hivyo, ni wazi Rais anapaswa kuzingatia miito ya Wakenya hao wote kwani matamshi yao yamekitwa kwenye nia ya kuleta hali ya utulivu nchini.

Katika mfumo wowote wa utawala, ni kawaida kwa tofauti kuibuka kati ya viongozi wa taasisi zilizopo.Hata hivyo, kilicho muhimu ni taratibu na njia zitakazotumiwa kusuluhisha tofauti hizo.Kwa mantiki hii, wito wetu kwa Rais Kenyatta ni kushusha msimamo wake mkali na kukubali miito iliyopo kuhusu haja ya kutatua mvutano huo.

Si picha nzuri wakati idara muhimu serikalini zinapovutana, hasa wakati uchaguzi mkuu unapoendelea kukaribia.Ombi letu kwa Rais Kenyatta na wadau wote husika ni kuanza utaratibu wa kuondoa mkwamo uliopo kwa manufaa ya Wakenya wote.

  • Tags

You can share this post!

Muungano wa kisiasa wa kaunti za Mashariki pigo kwa Mlima...

Mikakati ya kuvutia wawekezaji wa kigeni izingatie SME