• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:39 AM
Mikakati ya kuvutia wawekezaji wa kigeni izingatie SME

Mikakati ya kuvutia wawekezaji wa kigeni izingatie SME

Na MARY WANGARI

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Kenya ilipokea mkopo wa Sh80bilioni kutoka kwa Benki ya Dunia kwa lengo la kuimarisha juhudi za kukabiliana na janga la Covid-19 na kufadhili biashara ndogondogo nchini.

Iwapo zitatumika ipasavyo, fedha hizo bila shaka ni afueni kuu kwa wamiliki wawekezaji katika biashara ndogondogo na za wastan (SME) nchini, ambao wameathirika pakubwa kutokana na virusi vya corona ambavyo vimeyumbisha mifumo ya kiuchumi nchini na kimataifa kwa jumla.

Huku wawekezaji wakiwa na matumaini makuu, pana haja ya kuangazia kwa makini Mswada wa Fedha 2021 hasa kufuatia bajeti mpya iliyotangazwa Alhamisi na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.

Kando na kwamba mswada huo unasheheni mapendekezo yatakayomwathiri mwananchi wa kawaida kulingana na bajeti mpya ya 2021/2022, umeanzisha vilevile mikakati ya utozaji ushuru inayoambatana na viwango vya kimataifa, jambo ambalo litapiga jeki pakubwa wawekezaji katika (SME) nchini.

Mapendekezo katika Mswada wa Fedha 2021 yanajumuisha kupunguza kiwango cha ukwepaji kulipa ushuru miongoni mwa kampuni za kigeni, hali ambayo imeripotiwa kuigharimu Kenya mamilioni ya pesa kulingana na utafiti uliofanywa hivi majuzi na Mtandao kuhusu Haki ya Ushuru (TJN).

Kuanzishwa kwa sheria mpya zinazohusu kutoa makao ya kudumu kwa kampuni za kigeni ufafanuzi kuhusu umilisi wa kampuni, pamoja na sheria inayoelekeza mashirika ya kigeni kuwasilisha taarifa za mapato, ni miongoni mwa masuala yaliyopo katika mapendekezo ya mswada huo.

Japo mapendekezo haya yanaashiria nia njema na hususan kuvutia mashirika na wawekezaji wa kimataifa nchini Kenya, ni sharti wadau husika wawe waangalifu wasije wakaathiri zaidi SME nchini hasa wakati zinapokabiliwa na nyakati ngumu kiuchumi.

Baadhi ya mikakati iliyopendekezwa katika juhudi za kuvutia wawekezaji wa kigeni, huenda ikageuka jinamizi kuu kwa wamiliki wa SME nchini kwa kusababisha ushindani usio wa haki kuhusiana na kiwango cha malipo ya ushuru wa kuendesha biashara.

Uhalisia ni kuwa, wafanyabiashara nchini tayari wanakabiliwa na mzigo mzito kuhusu gharama kuu ya kufanya biashara na kuwawekea vikwazo zaidi vya kupata mikopo ya mtaji pamoja na kupandisha kiwango cha ushuru wanaotozwa ni sawa na kuwaangamiza kabisa.

Utafiti umeonyesha kwamba idadi kubwa ya wawekezaji nchini huendesha biashara zao kwa kutegemea mikopo kutoka kwa benki na taasisi mbalimbali za kifedha ili kufadhili shughuli zao.

Kutokana na mikakati ya kudhibiti Covid-19, wawekezaji wengi wamejipata katika njia panda huku wakilemewa na riba inayozidi kuongezeka ya mikopo waliyochukua nayo mapato yao yakiendelea kudorora na baadhi hata wakilazimika kufunga biashara zao.

Serikali inapojitahidi kuongeza mapato ya ushuru kwa kuvutia wawekezaji wa kigeni, haina budi kubuni mikakati kabambe na sera zitakazohakikisha kwamba wafanyabiashara wa humu nchini hawataathirika.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama: Ni wakati Rais akubali miito

Kivumbi balaa nusufainali ya ngarambe ya Betway Cup