• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Majengo ya mamilioni ya pesa Eldoret kubomolewa kuigeuza jiji     

Majengo ya mamilioni ya pesa Eldoret kubomolewa kuigeuza jiji    

NA TITUS OMINDE

MAJENGO yenye thamani ya mamilioni ya pesa mjini Eldoret na viunga vyake yaliyojengwa kwenye njia za mifereji ya majitaka na ardhi ya umma, yako kwenye hatari ya kubomolewa kufuatia mipango kuupa mji huo sura mpya.

Mji wa Eldoret unatarajiwa kupandishwa hadhi kuwa jiji.

Tayari majengo matano ya kibiashara katikati mwa mji yametengwa kwa awamu ya kwanza ya ubomoaji kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Manispaa ya Eldoret, Bw Julius Kitur alisema serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu pia inaangalia ubora wa majengo, jambo ambalo pia litatumika kama njia mojawapo kubomoa yale ambayo hayajaafikia kanuni za ujenzi.

Bw Kitur ameamuru wamiliki wa majengo ambayo kwa sasa yanaendelea kujengwa kusitisha miradi hiyo baada ya kubainika kuwa sio salama.

Alikuwa akizungumza na vyombo vya habari wikendi, baada ya kutembelea baadhi ya majengo yanayoyolengwa kubomolewa Eldoret huku akiwa ameandamana na Meneja wa Bodi ya Manispaa hiyo, Tito Koiyet.

Timu ya bodi ya manispaa inayoongozwa na Bw Kitur ilishangaa kubaini kwamba jengo la ghorofa mbili lililoathirika na linalomilikiwa na Fims Limited, liliundwa kwenye njia ya kupitishia maji.

Bw Kitur aliwataka wasimamizi wa kampuni hiyo kusitisha mara moja ujenzi unaoendelea kwenye kipande cha ardhi ambacho walidai ni cha serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu.

“Mjengo huu upo kwenye njia ya kupitisha majitaka na sisi kama kaunti hatutaruhusu kazi ya ujenzi kuendelea kwa sababu hii ni eneo la matumizi ya umma,” alisema afisa huyo.

Bw Koiyet, ambaye ni meneja wa bodi ya manispaa ya Eldoret alisema kuwa bodi hiyo tayari imechora ramani ya miundomsingi haramu na maendeleo ambayo haijaidhinishwa na ambayo alisisitiza kuwa itaporomoshwa.

“Bodi ya manispaa imeweka mikakati ya kubomoa miundo haramu iliyojengwa bila idhini kwenye maeneo ya umma. Mwekezaji yeyote anayejua kwamba alipata mali ya kaunti kwa njia za mkato anapaswa kujisalimisha kabla ya kutiwa mbaroni,” akaonya Bw Koiyet.

Hata hivyo, meneja wa Kampuni ya Fims, Francis Osoro alikanusha madai yaliyotolewa na mwenyekiti wa bodi kuwa ujenzi wa jengo la kampuni yake ni miongoni mwa maeneo yanayolengwa.

Bw Osoro aliwashutumu maafisa wa bodi ya Manispaa kwa kuwaamuru kusitisha kazi ya ujenzi inayoendelea katika eneo hilo, bila kuwapa nafasi kujieleza kuhusu suala hilo.

“Ni makosa kwa maafisa wa bodi ya manispaa kuvamia eneo la ujenzi bila hata kutufahamisha kuhusu lengo lao. Tumevamiwa na kuagizwa kusitisha kazi yoyote ya ujenzi inayoendelea ili tusije tukakabiliwa na adhabu ya bodi ya manispaa ya Eldoret,” akalalamika Bw Osoro.

  • Tags

You can share this post!

Uhalifu: Kilabu cha burudani Nairobi ambapo simu za walevi...

Papa ateua Muheria Kaimu Askofu wa Embu

T L