• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
Makahaba walilia serikali iwalinde dhidi ya dhuluma za wazee wa mitaa

Makahaba walilia serikali iwalinde dhidi ya dhuluma za wazee wa mitaa

Na WINNIE ATIENO

MAKAHABA mjini Mombasa wanaitaka serikali iwalinde dhidi ya dhuluma na unyanyasaji wanaopitia mikononi mwa wazee wa mitaa.

Wanadai wazee hao huwatoza Sh200 kwa kila mteja, huku wakishirikiana na vijana kuwadhulimu wanapokuwa kazini, hasa katika eneo la Nyali.

“Tunapigwa kila mara. Usalama wetu uko hatarini. Hatuna pa kukimbilia. Tukienda vituo vya polisi tunafukuzwa. Wakati wa kura huwa tunabembelezwa lakini sasa hatuna maana,” alisema mmoja wao, walipokusanyika jana mtaani Bombolulu.

Aidha, waliwalaumu wenye nyumba za wageni kwa kuongeza kodi ya ukahaba.

“Kitambo tulikuwa tunalipishwa Sh500 tukienda kukodi nyumba. Siku hizi wenye vyumba wanataka mtu alipe ada ya mteja na kahaba. Ukahaba umekuwa ghali sana na wateja wenyewe hawataki kulipa pesa. Kafyu imetuathiri sana hata hatupati faida yoyote,” alisema mwanachama mwingine aliyejitambulisha kuwa Bi Jane.

Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto watano alisema aliingilia sekta ya ukahaba kutokana na ukosefu wa kazi.

“Mume wangu aliniacha na watoto miaka 10 iliyopita. Ikabidi nisake riziki kwa njia yoyote. Lazima niwalishe, niwavishe na kuwaelimisha wanangu. Si kupenda kwangu kuwa kahaba,” akasema.

Mama huyo alisema huwa anatoza mteja Sh700.

“Wenzangu wametorokea miji mingine kama Diani na Mtwapa sababu ya unyanyasaji unaoendelea hapa Mombasa. Tunashangaa kwa nini mzee wa mtaa achukue pesa zetu. Nyakati zingine tunakosa hata wateja,” akalalama.

Kutokana na mamalishi yao, mwakilishi maalum wa wadi, Bi Fatma Kushe aliwasihi maafisa wa usalama kuwakamata wanaoendelea kuhangaisha makahaba hao.

“Si kupenda kwao, wanatafuta riziki. Kwa nini uwadhulumu? Wazee wa mtaa wanaojihusisha na tabia hii wanafaa kuchukuliwa hatua,” alisema Bi Kushe.

Aliwataka wanaume wasio katika ndoa watumie lugha nzuri wawatongoze na kuwaoa wanawake hao, badala ya kuwaacha kuendeleza biashara hiyo.

“Kama umefika umri wa kuoa heri uchukue mmoja wa hawa akina mama ili uwasitiri. Baadhi yao huenda wakawa wanawake wazuri tu kwa tabia, lakini wamesukumwa huku na matatizo,” akasema.

Pia alimtaka mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Asha Hussein kuwapa wanawake hao fedha za kufanya biashara.

You can share this post!

BBI: SAINI ZA UHURU, RAILA ZATUPWA

Macho yote kwa Haji kuhusu wizi wa mabilioni Kemsa