• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
BBI: SAINI ZA UHURU, RAILA ZATUPWA

BBI: SAINI ZA UHURU, RAILA ZATUPWA

Na LEONARD ONYANGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Alhamisi ilipata wakati mgumu kueleza kwa nini saini za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni miongoni mwa saini milioni 3.1 za kuunga mkono kura ya maamuzi ambazo zimetupwa nje katika orodha ya saini zilizothibitishwa kuwa halali.

Kati ya saini milioni 4.4 za kuunga mkono Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) zilizowasilishwa kwa IEBC ili zikaguliwe, ni saini milioni 1.3 tu zilizochapishwa kuwa bila dosari.

Majina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga pamoja na vigogo wengine wa siasa ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe BBI hayakuwa kwenye orodha hiyo iliyochapishwa na IEBC.

Baadhi ya vigogo ambao saini zao zilikosa ni kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi cha Cotu Francis Atwoli, katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju na mwenyekiti wa chama hicho tawala David Murathe.

Kwenye tangazo lililotiwa sahihi na Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, orodha ya majina iliyochapishwa katika mtandao wa tume hiyo ilinuiwa kutoa nafasi kwa yeyote mwenye malalamishi kwamba aliingizwa bila idhini, kuyawasilisha mapema.

Wananchi walipewa siku mbili pekee wawasilishe malalamishi, hadi Jumatatu saa kumi na moja jioni.

“Ripoti hii iliandaliwa kwa kuondoa majina yaliyokuwa na dosari kama vile yaliyokosa kuwa na saini, nambari ya kitambulisho au jina kamili,” alisema Bw Chebukati.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho ni miongoni mwa vigogo wa kisiasa wachache wanaounga mkono BBI ambao majina yao yako kwenye orodha hiyo.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya pia hayuko kwenye orodha hiyo. Mpigakura mwenye jina sawa na kiongozi huyo wa Kakamega, ameonyeshwa kuwa amesajiliwa kupiga kura katika Shule ya Msingi ya Kamagut Kipkeino, Kaunti ya Uasin Gishu.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa wa kwanza kutia saini zao wakati wa hafla ya kuzindua shughuli ya kukusanya saini kutoka kwa Wakenya iliyofanyika katika Jumba la KICC, Nairobi, mnamo Novemba 25, mwaka jana.

Wakati wa kuwasilisha saini hizo kwa IEBC, mwenyekiti mwenza wa Sekretariati ya BBI Dennis Waweru aliwataka makamishna wa tume hiyo kuwa waangalifu kwani ‘humu ndani kuna saini ya Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga’.

IEBC ilianza shughuli ya kukagua saini za BBI mnamo Desemba 30, mwaka jana na ilihusisha makarani 400 baada ya kutengewa Sh93 milioni.

Tume hiyo ilijaribu kujiondolea lawama kuhusu kukosekana kwa majina ya vigogo katika orodha ya wanaounga mkono BBI, lakini maelezo yao yakaibua maswali zaidi miongoni mwa wananchi.

Kwenye taarifa ya pili iliyotolewa na Bw Chebukati jana mchana baada ya wanahabari kufichua vigogo walitemwa, tume hiyo ilidai haijamaliza kukagua saini zote zilizowasilishwa kwake.

“Tume ingependa kufafanua kwamba shughuli za kuchunguza majina bado inaendelea na kama kuna yeyote anayeunga mkono (BBI) na majina yao hayapo katika orodha hii ya kwanza basi bado yanachunguzwa. Orodha kamili itachapishwa wakati shughuli itakapokamilika,” akasema.

Swali lililoibuka ni, kwa nini maelezo haya hayakuwepo katika tangazo la kwanza halisi ambalo lilionyesha kama kwamba shughuli nzima imekamilika, na kilichobaki ni kuondoa majina ya watakaolalamika pekee.

Hii si mara ya kwanza kwa tume hiyo kujikuta taabani kuhusu mipango ya kura ya maamuzi.

Wakati shughuli ya kuthibitisha sahihi ilipoanza, IEBC ilishambuliwa vikali iliporejelea BBI kama Mpango wa Kuteketeza Madaraja badala ya Mpango wa Kujenga Madaraja.

Zaidi ya hayo, uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kungali kuna dosari tele katika orodha iliyochapishwa jana.

Majina mengi yamerejelewa, na pia kuna majina ambayo si kamili. Kwa msingi huu, huenda idadi ya sahihi zitakazoidhinishwa ikawa ndogo zaidi.

You can share this post!

Makanisa yachomwa, ukuta wapakwa kinyesi Kisii

Makahaba walilia serikali iwalinde dhidi ya dhuluma za...