• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Makala ya msanii- Davy Dee

Makala ya msanii- Davy Dee

NA ABDULRAHMAN SHERIFF 

ALIKUWA na nia kubwa ya kuwa wakili kwa sababu ya kutaka kuwatetea wale wanaodhulumika kwa kukosa kuwakilishwa kutokana na ukosefu wa fedha. 

Lakini nia yake David Thoya almaarufu Davy Dee haikuweza kutimia kutokana na matatizo ya wazazi wake kupelekana mbio za kutaka kuepukana na hivyo, ilibidi akose kipindi kirefu cha masomo yake na kiushindwa kupata shahada ambazo zingelimuwezesha kusomea uwakili. 

Ilikuwa mwaka 2012 ndipo Davy Dee alipopatikana na kisanga kilichomkoroga maisha yake na hivyo alionelea kuwa na umuhimu wa kutuma ujumbe wa watu wa mitaani ambao huwa na uwezo mdogo wa kupeleka maisha yao. 

“Njia kubwa niliyofikiria ujumbe wangu utafikia watu wengi ni kujitosa kwenye fani ya kuimba ambapo nyimbo zitaweza kusikilizwa na wengi,” akasema msanii huyo chipukizi ambaye anaamini nyimbo zake zitapendwa kwa sababu zina mafunzo ya mashakil ya dunia. 

Davy alianza kwa kuimba mwaka 2008 akiwa shuleni na wenzake 27 katika kundi lilojulikana Max Melo ambalo lilikuwa la kuimba na kunengua. Kundi hilo lilitoa album mbili za nyimbo 14, kila album likiwa na nyimbo saba.  

Msanii Davy Dee PICHA/ABDULRAHMAN SHERIFF

Baadhi ya nyimbo za kundi hilo zilizopendwa zaidi ni pamoja na zile za ‘Simuachi’, ‘Holy’, ‘Achana na anasa’ na ‘Twasema asante’.  Kutokana na wengi wa wanachama wa kundi hilo kuoa na kuolewa, ilibidi Davy Dee aanze kufuata mweleko wake kimuziki. 

Ilikuwa mwaka 2015 ndipo msanii huyo alipotoa kibao chake mwenyewe cha ‘Sifa’ ambacho ndicho kilichomtambulisha na kumpa jina sio Mombasa pekee bali hata huko Nairobi, Kisumu, Uganda na Tanzania. 

“Niliuimba wimbo huo kwa sababu ya kumshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kufika mahali nilipofika kimuziki; nilitambua kwa kuimba wimbo huo wa ‘Sifa’ na kuitikiwa vizuri ilikuwa ni ufunguo mpya wa maisha yangu,” akasema Davy Dee.  

Aliporudi safari zake za Tanzania na Uganda mwaka huo wa 2015, alianza kutoa kibao kimoja hadi kingine huku akiwa anavutia mashabiki wengi zaidi waliokuwa wakimuunga mkono na kumsihi aendelee na Sanaa hiyo. 

Kati ya nyimbo zake alizowahi kuimba baina ya mwaka 2016 hadi sasa na ambazo nazo ziliitikiwa ni pamoja na zile za ‘Tembea na mimi’, ‘Bado’, ‘Tetanao’ na ‘Naanza nawe’ ambao ameuzindua mwanzo wa mwaka huu. 

Kwa wakati huu, Davy Dee anajitayarisha kuzindua albam yake ya nyimbo saba zikiwemo hizo. “Ninaazimia kuizindua albam hiyo hapo Agosti 8. “Nina uhakika album yangu hii itawapendeza mashabiki wangu pamoja na wapenzi wa muziki,” akasema. 

Nia yake kubwa ni kutaka kuwa na label yake ya muziki ili ipate kutambulika mbali na kutaka kufungua kituo cha watoto mayatima na wale ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalea na kuwa mwanaharakati wa kutetea maslahi ya wanyonge. 

Hapa nchini anapenda sana muziki wa Sarah K kwa sababu anasema mwana mama huyo anamkosha kutokana na kutokuwa na scandali yoyote kwa miaka yote nimemtambua.  “Mimi nina hamu ya kufikia viwango vya wanamuziki watajika wakiwemo kina Benjamin Dube, Uche wa Afrika Kusini.

Nawapenda sana wanamuziki kina Gloria Muliro, Bahati Bukuku wa Tanzania hali nchini Kenya nawapenda kina Emmy Kosgei, Eunice Njeri na Mr Gug,” akasema. Anawaambia mashabiki wake pamoja na wapenda muziki wote kuwa wazidi kumuunga mkono ili aweze kufikia malengo yake hasa ya kusimama na jamii.

  • Tags

You can share this post!

Shahbal asema bado hajaingia rasmi ODM

Kivumbi kikali kushushwa kwenye mechi za BNSL