• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:26 PM
Shahbal asema bado hajaingia rasmi ODM

Shahbal asema bado hajaingia rasmi ODM

Na ANTHONY KITIMO

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal anayepania kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao bado hajajiunga na Chama cha ODM rasmi, imefichuka.

Bw Shahbal ambaye amekuwa akiandaa mikutano mingi katika sehemu mbalimbali za Mombasa kwa maandalizi ya uchaguzi ujao alikuwa amehama Chama cha Jubilee miezi michache iliyopita, akatangaza atajiunga na ODM.

Tangu alipoondoka Jubilee, mfanyabiashara huyo amekuwa akikutana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga na pia naibu kiongozi Hassan Joho ambaye ni Gavana wa Mombasa, anapomezea mate tikiti ya chama hicho.

“Hivi karibuni nitapokelewa kama mwanachama wa ODM lakini hii ni shughuli ya kisheria ambayo bado inaendelea. Lazima tukamilishe hatua ya kwanza ambayo ni kumalizana na msajili wa vyama vya kisiasa, ndipo nielekee rasmi kuwa mwanachama wa ODM. Tayari nimeanza mashauriano kuhusu suala hili na viongozi wa ODM kitaifa na hapa Mombasa,” alithibitisha Alhamisi katika mahojiano na Taifa Leo.

Bw Shahbal anatarajiwa kupigania tikiti ya ODM kuwania ugavana dhidi ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Ujio wa Bw Shahbal ulionekana na wadadisi wa kisiasa kumharibia hesabu Bw Nassir ambaye angekuwa katika nafasi bora kupata tikiti ya moja kwa moja katika ODM kando na kupata uungwaji mkono kutoka kwa Bw Joho. Hata hivyo, Bw Nassir husisitiza hahitaji kushikwa mkono na kigogo yeyote wa kisiasa kwani anaamini wananchi watachagua viongozi kwa msingi wa utendakazi wao. Wawili hao wamekuwa wakijizatiti kujitafutia umaarufu kwa viongozi wakuu wa ODM.

Wiki hii, Bw Shahbal alisafiri kwa ndege moja na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt Oburu Oginga ambaye ni nduguye Bw Odinga kwa hafla Kaunti ya Murang’a.

Bw Shahbal alisema alihudhuria hafla hiyo kufuatia mwaliko kutoka kwa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Madai polisi walipata mamilioni kwa majaji

Makala ya msanii- Davy Dee