• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mamia ya wakazi Mukuru kupoteza makao kupisha ujenzi wa hospitali

Mamia ya wakazi Mukuru kupoteza makao kupisha ujenzi wa hospitali

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

MAMIA ya wakazi katika mtaa mmoja wa mabanda watapoteza makao yao ili kuipa serikali nafasi ya kujenga hospitali ya umma.

Akiongea na Taifa Leo jana, mwakilishi wa wodi ya Viwandani, kaunti ya Makadara, Bw David Mbithi alisema mipango ni kamilifu ya kujenga hospitali ya Level 2 katika mtaa wa Mukuru-Jamaica.

Aidha, Bw Mbithi aliongeza kuwa lengo ya serikali ni kuwajengea wakazi hospitali ya umma mashinani na kuwapunguzia mzingo wa kusafiri mwendo mrefu kusaka huduma hiyo kutoka Hospitali ya Mama Lucy na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

“Nia ya serikali ilikuwa ni kuwapumzishia wakazi mitaani ya mabanda mzigo wa kusafiri kilomita nyingi kwenda kutibiwa katika hospitali ya Mama Lucy na Hospitali Kuu ya Taifa ya Kenyatta,’’ Bw Mbithi akasema.

Fauka ya hayo, hospitali hiyo inatazamiwa kuwafaidi wakazi katika mitaa tano ya mabanda ilioko kwenye tarafa ya Viwandani.

Miongoni mwa mitaa hiyo ni pamoja na mtaa wa mabanda wa Mukuru-Lunga Lunga, Mukuru-Jamaica, Mukuru-Sinai, Mukuru- Paradise na Mukuru-Cereals.

Hata hivyo, alisema ili maendeleo hayo yapatikane, watu kadhaa watapoteza makao yao kupeana nafasi ya kujengwa kwa hospitali hiyo.

Zaidi ya hayo, watakaoathirika watapatiwa nyumba badala kwenye Mpango wa Nyumba Yangu.

Kufikia sasa, wakazi wamehamasishwa kuhusu mpango wa ujenzi ya hospitali pamoja na mipango ya jinsi watakaopatiwa makao mengine bila vurugu.

Nyumba zilizoratibiwa kupewa waathiriwa watakaohamishwa zimo mtaani Makongeni, Mbotela na Pangani.

’’Tayari serikali imejenga nyumba zitakazopatiwa watakaoathirika kutoka mtaa wa Mukuru-Jamaica. Watu watapewa nyumba na serikali katika mtaa wa Makongeni, Mbotela na mtaa wa Pangani,” Bw Mbithi alisema.

Kwa kawaida wakazi wa mitaa ya mabanda katika eneo la Viwandani, kaunti ya Nairobi huhudumiwa katika zahanati ya Mareba inayosimamiwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi.

‘’Watu wa Mukuru katika tarafa ya Viwandani hutafuta huduma ya matibabu katika zahanati ya Mareba fauka ya watu kuongezeka kila siku. Kuna umuhimu wa kujenga hospitali kubwa ya umma, iliyo karibu na watu wakati huu wa ugatuzi,’’ Bw John Otieno, mwenyekiti wa usalama mtaani katika mtaa wa Jamaica asema.

  • Tags

You can share this post!

Fursa ya Olunga kung’ara Kombe la Dunia la Klabu ni...

Mean Machine na Egerton Wasps waanza kufukuzia tiketi ya...