• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Mandazi aina ya ‘kangumu’ yamtia gavana wa Nyandarua hofu

Mandazi aina ya ‘kangumu’ yamtia gavana wa Nyandarua hofu

Na STEVE NJUGUNA

GAVANA Francis Kimemia wa Nyandarua, ameingiwa na wasiwasi kutokana na idadi kubwa ya wakazi kula mandazi kupindukia.

Bw Kimemia alisema ulaji mwingi wa mandazi hasa miongoni mwa watoto na wazee, umechangia ongezeko la utapiamlo katika kaunti yake.

“Nini kinapatikana kwa hii mandazi aina ya ‘kangumu’ kiasi kwamba yanapendwa sana na watoto pamoja na wazee wa kaunti yetu?” akauliza gavana huyo.

Gavana huyo alisikitika kwamba wakulima wengi huwakama ng’ombe wao kisha kuuza maziwa yote bila kuwapa watoto wao.

Aliwashauri wazazi wawape watoto wao vyakula vyenye protini ili kusaidia kumaliza utapiamlo.

Alisema kaunti hiyo ni kati ya zile zinazokabiliwa na utapiamlo kwa kuwa watoto wengi wamechangamkia mandazi badala ya mayai yanayopatikana kwa urahisi eneo hilo.

Alieleza masikitiko kuwa watoto wengi wanaendelea kukabiliwa na utapiamlo ilhali wazazi wao wanashiriki kilimo na ufugaji.

“Utapiamlo katika baadhi ya maeneo ya Nyandarua ni zaidi ya asilimia 29 hasa katika eneobunge la Ndaragwa,” akasema.

“Hakikisheni watoto wenu wanakula mayai na nyama ya kuku badala ya kushinda kila siku wakila mandazi, viazi na mkate. Kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, kaunti inaweka mikakati kuhakikisha tunapata nyama ya kuku,” akasema Bw Kimemea.

You can share this post!

Wabunge watisha kuvuruga usomaji bajeti Alhamisi

Vitengo vinne vikuu kuwakabili polisi watendao maovu