• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
Maoni mseto mitandaoni DCI ikianza kutumia Kiswahili kusimulia matukio

Maoni mseto mitandaoni DCI ikianza kutumia Kiswahili kusimulia matukio

Na WANGU KANURI

[email protected]

BAADA ya Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuchapisha kuwa itakuwa ikielezea matukio kwa Kiswahili, baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii wameshangazwa na misamiati inayotumika huku wengine wakieleza kuwa hawaelewi kinachoandikwa.

Waliochangia masimulizi yanayochapishwa na DCI wamezionyesha hisia tata huku wengine wakiridhishwa na tangazo hilo na wengine wakilalama.

DCI ilianzia matoleo ya Kiswahili ya simulizi za uhalifu yanayochapishwa kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii, baada ya kuona haja ya kuwasiliana vyema na watu wote katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Hii ni hatua nzuri. Kuendesha shughuli kwa Kiswahili katika korti, kutumika kwenye stakabadhi rasmi, bungeni na kadhalika ni muhimu. Wahitimu wa Kiswahili watapata kazi za utafsiri wa faili na hotuba,” akaeleza James Wachira kupitia Facebook.

“Kazi nzuri! Hivi sasa ninafurahia sana kuzisoma ripoti hizi za matukio ya uhalifu kwa Kiswahili,” akasema Roselyn Makona kupitia Facebook.

“Vizuri mno. Heko!” akasema @VOA_Wandera kupitia Twitter.

“Kiswahili kinapaswa kupewa nafasi ya juu katika jamii. Wananchi wana haki ya kupata habari kwa lugha ya Kiswahili,” akaandika @kairu_karega.

“Tafadhali kusoma simulizi hizi kwa Kiswahili inachukua muda. Heri Kiingereza,” akasema Ericsson Likhanga kupitia Facebook.

Kiswahili kitukuzwe lakini ni kigumu sana kukisoma na kukielewa,” akaandika Wangari Macharia kupitia Facebook.

“Jokofu??” @jerrykitur01 akashangaa baada ya kusoma chapisho moja la DCI lililoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

“Jokofu… kipakatalishi…” akaandika @IndekuJoseph baada ya kusoma kwenye ukurasa wa Twitter wa DCI.

You can share this post!

Afueni wakazi wa Carwash-Zimmerman wakiimarishiwa barabara

TANZIA: Mtangazaji Badi Muhsin afariki