• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Dereva wa teksi aliyekula Sh40,000 za karao ajutia kitendo chake akiwa nyuma ya nondo

Dereva wa teksi aliyekula Sh40,000 za karao ajutia kitendo chake akiwa nyuma ya nondo

NA MWANGI MUIRURI

MURANG’A

POLO dereva wa teksi aliyekula Sh40,000 za karao wa Murang’a sasa anajutia kitendo chake akiwa kwenye rumande akisaka wa kumfanyia harambee amlipie.

Kwa mujibu wa mdokezi wa meza ya dondoo, polisi huyo alikuwa amekodisha huduma za teksi polo amsafirishe hadi mji wa Sagana kutoka Murang’a Mjini kwa ada ya Sh800.

“Polisi huyo wa kiume alilipa Sh400 katika kituo cha mafuta cha Astrol kilichoko mjini Murang’a ahadi ikiwa wakifika Sagana angemlipa Sh400 zilizosalia,” mdokezi akasema.

Polo aliendesha gari na akamfikisha karao mjini Sagana na ambapo malipo yalifanyika kupitia simu ya mkononi.

“Karao alikuwa ametei akatuma Sh40,000 badala ya Sh400. Polo akachomoka eneo hilo la kulipiwa kana kwamba alikuwa anatoroka mauti,” akasema mdokezi.

Polisi naye alikuja kuelewa balaa aliyojitwika baada ya siku moja na alipopiga simu kwa polo kujua kulikoni, akapata imezimwa.

Kumbe naye polo wa teksi aliingia mitimi kuponda raha ambapo alikuwa tu akionekana kwenye sehemu za kuuza pombe na nyama huku akila maisha na kujienjoi na vidosho.

Kwa kifupi, Sh40,000 zikielekezwa kwa raha ya kiwango hicho haziwezi zikadumu mkobani kwa siku zilizo na heshima. Ziliisha.

“Ndipo polo alirejea katika steji yake ya huduma za teksi na muda si muda, polisi wakaingia na akawekwa pingu. Aliwasilishwa hadi kituo cha polisi mjini hapa na akashtakiwa katika mahakama  kwa kosa la wizi,” asema mdokezi.

Polo kufika mbele ya hakimu akiwa na uoga wake ukiambatana na ‘kutojua ujanja wa kesi’, akakiri kwamba alikula pesa za polisi.

“Lakini aliomba hakimu ampe wiki moja atafute pesa hizo ili azirejeshe na akatumwa rumande ili asake mbinu ya kulipa. Mamake mzazi amefichua kwamba amepata Sh30,000 hadi sasa huku kukibakia siku tatu pekee makataa ya mahakama kutimia,” akasema mdokezi.

Karao huyo kwa sasa anasikika mtaani akiapa kwamba pesa zake si za kuchezewa na kuna gharama ya kujaribu kumtapeli.

  • Tags

You can share this post!

Mtundu Sasha Obama apigwa picha akivuta bangi

Mapato ya wafanyakazi kuendelea kunyofolewa

T L