• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Echesa alikuwa amemletea Ruto Wazungu wawili alipokamatwa, korti yaambiwa

Echesa alikuwa amemletea Ruto Wazungu wawili alipokamatwa, korti yaambiwa

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia na Michezo Rashid Echesa alitiwa nguvuni baada ya kuondoka katika afisi ya Naibu wa Rais William Ruto ambapo alikuwa amewapeleka Wazungu wawili kumwona, mahakama ilifahamishwa Jumatatu.

Akitoa ushahidi mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot, mlinzi wa Dkt Ruto, Bw Nicholas Maiyo Burkley, alisema Wazungu hao wawili walikuwa wamebeba mfuko.

Bw Maiyo alisema aliwapeleka wageni hao wa Dkt Ruto katika chumba cha mapokezi wamsubiri kwa “vile hakuwa ameingia afisini siku hiyo.”

Bw Maiyo , aliyefichua amekuwa mlinzi wa Dkt Ruto tangu alipokuwa Waziri wa Kilimo, alisema alimwuliza Bw Echesa, ikiwa Naibu wa Rais alikuwa akiwatarajia walipofika afisini mwake mnamo Februari 13 2020.

“Bw Echesa alinieleza Dkt Ruto alikuwa akiwasubiri,” Bw Maiyo alisema.

Bw Maiyo ambaye amehudumu katika kikosi cha Polisi kwa miaka 14 sasa alisema “Nilichukua simu za Wazungu hao pamoja na mfuko waliokuwa wamebeba. Sikuchukua simu za Bw Echesa kwa vile alikuwa anazitumia kuwasiliana na Dkt Ruto ambaye hakuwa amefika afisini siku hiyo.”

Alisema pia aliwasiliana na afisi ya Dkt Ruto iliyokuwa katika makazi yake rasmi yaliyoko mtaani Karen, Nairobi.

“Niliwasiliana na maafisa katika afisi ya Dkt Ruto iliyoko Karen walionieleza hatafika afisi iliyoko jijini kwa vile alikuwa anahudhuria mazishi Kandara kaunti ya Murang’a,” alisema Bw Maiyo.

Mahakama ilielezwa Bw Echesa alishauriwa awasiliane na afisi ya Karen.

Bw Maiyo alisema aliwarudishia wazungu hao simu zao za kiunga mbali pamoja na mfuko wao kisha akawaelekeza kutoka afisi ya naibu wa rais.

Shahidi huyo alisema hatimaye alifahamishwa Bw Echesa alitiwa nguvuni kwa kula njama za kumlaghai mwekezaji Kozlowski Stanley Bruno zaidi ya Sh40 bilioni katika kashfa ya silaha katika idara ya ulinzi (DoD).

Echesa ameshtakiwa pamoja na Daniel Otieno Omondi almaarufu General Juma, Clifford Okoth Oanyango almaarufu Paul na Kennedy Oyoo Mboya.

Wote wameshtakiwa kula njama z akumlaghai Bw Bruno mabilioni hayo kwa njia ya undanganyifu.

You can share this post!

Wanaume wa Kenya wajikwaa dhidi ya Nigeria voliboli ya...

Maskwota elfu tatu wafurushwa