• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Mbunge wa Mathare ashtakiwa baada ya ‘kuzungushwa hii town’

Mbunge wa Mathare ashtakiwa baada ya ‘kuzungushwa hii town’

NA RICHARD MUNGUTI

BAADA ya kuwazuilia na kuwaficha kwa siku nne mfululizo, polisi hatimaye waliwafikisha kortini Mbunge wa Mathare Antony Oluoch na aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga.

Haya yakijiri Polisi walimtia nguvuni Spika wa Bunge la Kaunti ya Makueni Bw Douglas Mbilu.

Bw Mbilu alipelekwa mahala kusikojulikana anakobanwa.

Kushtakiwa kwa Oluoch, Njenga na madiwani Peter Imwatok na Alvin Olando Palapala kulituliza nyoyo za watu wafamilia zao.

Baadhi ya jamaa za washtakiwa hawa waliambia Taifa Leo mahakamani, “sasa tunajua wako hai.”

Mnamo Jumapili baba yake Maina Njenga Bw Stephen Kamunya Njoroge alitoa wito kwa serikali iwaachilie au kuwashtaki wanawe wawili badala ya kuwazuilia kinyume cha sheria.

Mbali na Oluoch na Njenga, madiwani wawili Peter Imwatok (Makongeni) na Alvin Olando Palapala (Kitsuru) pia walishtakiwa.

Njenga alishtakiwa katika Mahakama ya Makadara ilhali Oluoch, Imwatok na Palapala walishtakiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Oluoch, Imwatok na Palapala walishtakiwa kwa kosa la kuandaa wakazi wa Nairobi kukaidi amri na kushiriki katika maandamano mnamo Julai 6 na 19, 2023.

Watatu hao walikana waliwashawishi wananchi kushiriki katika maandamano ya Julai 7 na 20-22, 2023 kinyume cha sheria ya utangamano.

Njenga alishtakiwa pamoja nduguye Peter Kamunya na Felix Ratu Lakishe mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Makadara Bw Francis Kyambi.

Watatu hao waliowakilishwa na wakili Harun Ndubi walikabiliwa na mashtaka ya kupatikana na silaha , dawa za kulevya na kujiandaa kutekeleza uhalifu.

Njenga na wenzake walikana kuwa mnamo Julai 19, 2023 katika eneo la Kiserian walikutwa na polisi wakiwa na  panga 14,  njora za kimasai 24 na rungu 46.

Mbali na silaha hizo, washtakiwa hao walikabiliwa na shtaka la kupatikana na gramu 1224 za bhani nba gramu 486 za Cocaine.

Polisi walidai watatu hao walikuwa wanajiandaa kutekeleza uhalifu.

Washtakiwa hao waliomba waachiliwe kwa dhamana wakisema wamekuwa kizuizini tangu Julai 19, 2023 walipotiwa nguvuni.

Upande wa mashtaka ulipinga wakiachiliwa kwa dhamana ukidai watavuruga uchunguzi na mashahidi.

Bw Kyambi atatoa uamuzi leo ikiwa atawaachilia kwa dhamana au la.

Katika kesi ya Oluoch,Imwatok na Palalala mawakili 20 wakiongozwa na rais wa chama cha wanasheria nchini LSK Eric Theuri aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana akisema “nchi hii imetumbukia katika utawala wa kiimla ulioshuhudiwa miaka ya 70 na 80 ambapo wapinzani wa serikali walikuwa wanatekwa nyara n ahata wengine  kuuawa.”

Bw Theuri alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina inasikitisha kuona wakuu serikalini wanaongea kiholela na kuidharau mahakama.

Kinara huyo wa LSK alisema: “Polisi walikaidi maagizo ya Mahakama Kuu wasiwatie nguvuni Imwatok na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.”

Lakini pasi kujali ,polisi walimkamata Imwatok na kumzuilia licha ya kuachiliwa kwa dhamana na Jaji Asenath Ongeri.

“Polisi na baadhi ya wakuu serikalini wameingiwa na tabia kukandamiza wananchi kwa kuwaua na kuwajeruhi pasi na sababu.”

Bw Theuri alisema polisi walimzuilia Bw Oluoch kwa siku nne na hawakuruhusu wakili au mtu wa familia yake kumfikia.

“Bw Oluoch alizuiliwa bila ya kukubaliwa kumeza dawa na pia hawakumpa chakula,” Bw Theuri alisema.

Wakili huyo aliomba mahakama itoe agizo kwa polisi watii sheria na maagizo ya mahakama.

“Inasikitisha na kuudhi kwamba polisi wanakaidi agizo la Mahakama kuu. Naomba mahakama iwaamuru endapo wanahitaji kumhoji mtu yeyote wamwite kwa njia ya kisheria na ustaarabu na kumhoji badala ya kuwateka nyara,” Bw Theuri alisema.

Lakini Bw Onyina hakutoa agizo lolote dhidi ya polisi ila aliwashauri mawakili wawasilishe madai katika mahakama kuu na kuomba wahusika wachukuliwe hatua kali.

Bw Onyina aliwaachilia Oluoch na Imwatok kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 kila mmoja naye Palapala akapewa dhamana ya Sh70,000.

Hadi pale tulipokuwa tunaenda mitamboni Bw Mbilu haikujulikana ni wapi alikuwa akizuiliwa.

Kesi dhidi ya Oluoch, Imwatok na  Palapala zitatajwa Agosti 8, 2023.

Upande wa mashtaka uliagizwa uwape washtakiwa nakala za mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Mabunge ya Kenya na Australia kushirikiana kiutendakazi

Ninaona udikteta Kenya, adai Raila

T L