• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Mhubiri Paul Mackenzie asusia chakula kizuizini

Mhubiri Paul Mackenzie asusia chakula kizuizini

NA ALEX KALAMA

IMEBAINIKA ya kwamba tangu kuanza kufanyika kwa operesheni ya kuchunguza makaburi ambayo ndani walizikwa watu walioaga dunia baada ya kufunga na kudhoofika kiafya kupindukia kwa kufuata mafundisho tata, mchungaji Paul Mackenzie amesusia chakula siku nne kizuizini.

Kulingana na ripoti kutoka kwa mmoja wa maafisa wa upelelezi, ni kuwa mhubiri huyo alianza kufunga siku nne zilizopita.

“Baada tu ya sisi kuanza hii operesheni ya kuchunguza maziko ya waliokuwa wafuasi wake, alianza kufunga. Kufikia sasa ana siku nne  hali wala hanywi maji. Ukimuuliza ni kwa nini hutaki kula wala kunywa maji anasema yuko kwa mfungo,” amesema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa haruhusiwi kuongea na wanahabari.

Mackenzie ambaye alikamatwa mnamo Ijumaa, Aprili 15, 2023, alifikishwa mahakamani Aprili 17, 2023 na kuzuiliwa katika kituo cha polisi kwa siku 14 huku uchunguzi ukiendelea ili kubainisha hasa kilichotokea Shakahola katika Kaunti ya Kilifi. Kesi hiyo itatajwa tena Mei 2, 2023.

Jana Ijumaa operesheni iliendelea ambapo maafisa walipochimbua shimo la kwanza walipata miili miwili ikiwa imezikwa na gunia katika kijiji kiitwacho Bethlehemu Yuda ndani ya msitu wa Shakahola.

Katika kaburi hilo la kwanza lililotanguliwa kufukuliwa walipata mama na mtoto wake wakiwa wamezikwa pamoja.

Huku kwenye kaburi la pili wakipata mwili mmoja wa mtoto. Ufukuaji makaburi ili kutoa miili bado unaendelea.

Afisa wa idara ya watoto eneo la Pwani Paul Migosi ana hofu kwamba huenda idadi kubwa ya mili itakayotolewa katika makaburi hayo ikawa ni ya watoto.

Vilevile katika operesheni hiyo pia maafisa mnamo Ijumaa waligundua kaburi moja kubwa linaloshukiwa kuzikwa miili zaidi ya 20.

Idadi ya watu walioaga na miili yao kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Malindi kufikia sasa ni miili minane mbali na ile mitatu ambayo ilifukuliwa jana Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yalaumiwa kwa kunyamaza watu wakiangamia Shakahola

Mali ya Tuju kupigwa mnada kutokana na deni la Sh2.2 bilioni

T L