• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Mifuko ya supa ya Mulei ilikutwa ndani ya nyumba ya afisa wa polisi anayeshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willie Kimani

Mifuko ya supa ya Mulei ilikutwa ndani ya nyumba ya afisa wa polisi anayeshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willie Kimani

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu ilifahamishwa jana mifuko ya kubebea bidhaa iliyokuwa na chapa cha Mulei Supermarket ilikutwa ndani ya nyumba ya afisa mmoja kati ya polisi wanne wanaoshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willie Kimani,mteja wake na dereva wa teksi miaka mitano iliyopita.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Jessie Lesiit , Inspekta Clement Mwangi alisema mnamo Julai 4, 2016 polisi walifanya msako ndani ya nyumba ya Sajini Leonard Mwangi na kupata mifuko ya Mulei Supermarket.

Bw Mwangi alisema mifuko hiyo ilifanana na ile iliyokuwa imewekwa kwenye vichwa vya wakili Kimani , Josephat Mwenda na Joseph Muiruri miili yao ilipopatikana katika mto Athi River eneo la Donyo Sabuk kaunti ya Machakos.

Maiti zao zilipatikana baada ua wiki moja zikiwa zimewekwa ndani ya magunia na vichwa kuvishwa mifuko ya Mulei Supermarket.Maiti hizi ziliguduliwa na mwanaume aliyekuwa ameenda mtoni kuoga.

Sajini Mwangi ameshtakiwa pamoja na Inspekta Fredrick Leliman, Stephen Cheburet Morogo , Sylvia Wanjiku Wanjohi na Peter Ngugi kwa mauaji ya  Kimani , Mwenda na Muiruri mnamo Juni 23, 2016 katika eneo la Soweto Mlolongo.

Maafisa wa polisi Fredrick Lelimani..(kushoto) , Stephen Chebureti (kati) na wakili Cliff Ombeta wakiwa kortini Jumanne…Picha/RICHARD MUNGUTI

Inspekta Mwangi alisema mbali na mifuko hiyo , pia polisi walipata shuka nyekundu ya  Kimaasai na redio ya polisi.Insp Mwangi alisema pia walipekua nyumba za maafisa wengine wa polisi Wilson Kamau Juma na Charles Waweru na hawakupata chochote cha kuwahusisha na mauaji ya watatu hao.

Sajini Mwangi alikuwa naibu wa Inspekta Lelimani katika kitengo cha polisi wa kupiga doria wakiwa wamevalia sare za umma almaarufu SPIV.

Insp Mwangi kutoka makao makuu ya idara ya kupambana na uhalifu (DCI) alichunguza kesi ya mauaji hayo alimweleza Jaji Lesiit walichukua shuka hiyo ya Kimaasai kwa vile afisa mwingine wa polisi Bw Paul Mitambo alimpata Leonard katika eneo la mauaji ya watatu hao usiku wa Juni 23,2021, akiwa amejifunika kichwani.

“Bw Mitambo anayeishi katika eneo la Soweto Mlolongo aliwakuta maafisa wa polisi katika eneo walipouliwa watatu hao kisha wakamwambia walikuwa wanavizia wahalifu,” Inspekta Mwangi alieleza korti.

Bw Mutambo anayefanya kazi katika kituo cha kupima uzani wa malori ya kusafirisha bidhaa alijulishwa washtakiwa na Landiledi wake Bi Agnes Wayua.Shahidi huyo alisema uchunguzi uliofanyiwa Redio ya Polisi aliyokuwa amepewa Bw Leliman ulionyesha alikuwa katika eneo la Soweto kuanzia saa moja unusu hadi saa sita usiku Juni 23, 2016.

Pia alisema maafisa hao wa SPIV hawakuwa kazini usiku huo Kimani na wenzake walipouawa.Waliposhikwa  Lelimani, Chebureti na Sylvia walikanusha walihusika na kutoweka na hatimaye kuuawa kwa Kimani , Mwenda na Muiruri.

Mahakama ilifahamishwa Mwenda alikuwa amelalamika kwa mamlaka huru ya utenda kazi ya polisi (IPOA)  na International Justice Mission (IJM) kwamba alikuwa anaonewa na Lelimani ambaye alikuwa amemtishia maisha na hata alikuwa amemfungulia kesi ya trafik na kupatikana na mihandarati.

Mnamo Juni 23, 2016  Mwenda alikuwa afike kujibu mashtaka katika mahakama ya Mavoko , Athi River kaunti ya Machakos.Watatu hao walitekwa nyara na kuzuiliwa katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau.

Waliripotiwa kupotea na hatimaye maiti zao zikapatikana zimetupwa mto Athi River.Kesi itaendelea kusikizwa leo.

  • Tags

You can share this post!

Uefa yapinga pendekezo la fainali za Kombe la Dunia...

Griezmann abeba Ufaransa dhidi ya Finland