• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 1:50 PM
Miili ya wavulana watatu yapatikana kwenye kidimbwi Juja

Miili ya wavulana watatu yapatikana kwenye kidimbwi Juja

NA LAWRENCE ONGARO

WAVULANA watatu wa kijiji cha Muthara, Juja, kaunti ya Kiambu, waliokuwa wametoweka wamepatikana wakiwa wamefariki dunia.

Miili ya watatu hao wa umri wa kati ya miaka sita na 10 ilipatikana Jumatano mchana kwenye kidimbwi kilichojaa maji karibu na eneo la shughuli za uchimbaji mawe.

Kulingana na wakazi wa kijiji hicho, mvua kubwa inayonyesha imesababisha maji kutuwama kwenye vidimbwi kadha.

Bw Joseph Maina mkazi wa hapo alisema walipata habari kuwa kuna vijana watatu walipatikana wakielea kwenye kidimbwi hicho bila kutambulika kamili.

Baadaye ndipo wakazi hao walifika hapo na kufanya juhudi za kuwaondoa vijana hao ndani ya kidimbwi hicho.

“Tunaomba watu wanaohusika na uchimbaji wa mawe wawe makini kuona ya kwamba mashimo yanayoachwa wazi yanajazwa mchanga ili kusitokee tena janga kama hilo,” alisema Bw Maina.

Bi Margret Wairimu aliye mkazi alisema mmoja kati ya vijana hao alipatikana alielea juu ya maji ya kidimbwi hicho lakini hao wengine wawili kuwaondoa wawili wengine walipatikana ndani ya matope baada ya wakazi kuzibua maji yaliyokuwa yametuwama.

Naye Elizabeth Wanjiku alidai ya kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kuwa maeneo ya kuchimba mawe yamekuwa hatari kwa usalama lakini hakuna hatua yoyote imechukuliwa.

“Tungetaka serikali ya kaunti ya Kiambu kuingilia kati ili kuzuia maafa ya aina hiyo kushuhudiwa tena,” alisema Bi Wanjiku.

Miili ya watatu hao ilipekekwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago katika Hospitali ya Thika Level 5.

Chini ya miezi sita iliyopita watu watano wamepoteza maisha yao katika eneo hilo la uchimbaji wa mawe.

Na mwaka 2021 wachimbaji mawe wawili na dereva walifariki katika eneo la uchimbaji mawe Juja baada ya eneo fulani kuporomoka.

Aidha, wakazi wa kijiji hicho wanaiomba serikali ya kaunti ya Kiambu iweke ua kuzingira eneo hilo ili lisiwe hatari kwa maisha ya binadamu.

  • Tags

You can share this post!

Jesse Lingard aamua kuondoka Man-United mwishoni mwa msimu...

Siri kuokoa nyanya zinazopotelea shambani na kwenye masoko

T L