• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Jesse Lingard aamua kuondoka Man-United mwishoni mwa msimu huu

Jesse Lingard aamua kuondoka Man-United mwishoni mwa msimu huu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Jesse Lingard amefikia maamuzi ya kuagana na Manchester United mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22 baada ya kuhisi kwamba hajathaminiwa na waajiri wake katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Mkataba wa sasa kati ya Man-United na Lingard unatamatika rasmi mnamo Juni 2022 na sogora huyo mwenye umri wa miaka 29 anawaniwa pakubwa na klabu za AC Milan, Juventus na Paris St-Germain (PSG).

Ingawa kocha mpya wa Man-United, Erik ten Hag ametaka kuzungumza na Lingard, nyota huyo raia wa Uingereza amepuuza mpango huo na kusisitiza kwamba hakuna kitakachomsadikisha kusalia ugani Old Trafford baada ya kampeni za muhula huu kukamilika.

Kwa mujibu wa Lingard, Man-United walimnyima fursa ya kujikuza kitaaluma kwa kujiunga na kikosi kitakachoshiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2022-23.

“Klabu ilinidanganya na kocha wa zamani, Ole Gunnar Solskjaer naye akanihadaa. Sawa na mkufunzi mshikilizi Ralf Rangnick, vinara wa benchi ya kiufundi waliahidi kunichezesha katika idadi kubwa ya mechi. Yasikitisha kwamba ahadi hiyo haikutimizwa,” akasema Lingard aliyechezea West Ham United kwa mkopo mnamo 2020-21.

Lingard amewajibishwa na Man-United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara mbili pekee msimu huu na aliachwa benchi katika mechi iliyopita iliyoshuhudia Man-United ikitandika Brentford 3-0. Mechi hiyo ilikuwa iwe ya mwisho kwa Lingard kuchezea Man-United ugani Old Trafford alikoanza kusakata kabumbu akiwa na umri wa miaka saba.

Lingard amechezea Uingereza mara 32 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na miamba hao kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar mnamo Septemba na Oktoba 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Wadau wa utalii Pwani wawe wabunifu...

Miili ya wavulana watatu yapatikana kwenye kidimbwi Juja

T L