• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Mkazi wa Nairobi apinga uchaguzi wa ugavana

Mkazi wa Nairobi apinga uchaguzi wa ugavana

Na RICHARD MUNGUTI

MKAZI na mpigakura katika Kaunti ya Nairobi amewasilisha kesi kupinga uchaguzi wa ugavana Nairobi kufuatia kutimuliwa kwa Gavana Mike Sonko.

Bw Josephat Kariuki Ng’endo anaomba Mahakama Kuu ifutilie mbali uchaguzi huu mdogo wa Ugavana utakaofanyika Februari 18, 2021.

Katika kesi iliyowasilishwa chini ya sheria za dharura na wakili Kiongora Mugambi, Bw Ng’endo asema kabla ya uchaguzi huu kufanyika, hatma ya naibu wa Gavana, Bi Anne Kananu Mwenda yapasa kujulikana.

Mlalamishi alisema ilani ya IEBC kwamba uchaguzi mdogo wa kujaza pengo lililoachwa na Bw Sonko ufanywe limezua utatanishi kwa vile haijaamua ikiwa itamchunguza Bi Mwenda au la. Uhalali wa uteuzi wa Bi Anne Kananu Mwenda ulipingwa kortini na mwanaharakati Peter Odhiambo Agomo.

Bw Agomo alihoji mamlaka ya Bw Sonko kumteua Bi Mwenda na jina lake kupelekwa kukaguliwa na IEBC kabla ya kuchapishwa rasmi katika Gazeti la Serikali.

Naye Bw Ng’endo katika kesi aliyowasilisha jana anaomba aruhusiwe kushiriki katika kesi hiyo ya Bw Agomo ikitiliwa maanani Bw Sonko aling’atuliwa wadhifa wa Ugavana na Bunge la Seneti na wadhifa wa Ugavana wa Nairobi kikatangazwa wazi Desemba 17, 2020.

Mnamo Desemba 21, 2020, Spika wa Bunge la Nairobi Bw Benson Mutura aliapishwa kuwa Gavana mwandamizi kwa siku 60.

Bw Ng’endo anaomba Mahakama Kuu isitishe uchaguzi huo mdogo na uteuzi wa Bi Anne Kananu Mwenda uhalalilishwe na mahakama au ufutiliwe mbali.

Mbali na kupinga uchaguzi huo mdogo Bw Ng’endo anaomba IEBC izuiliwe kumhoji Bi Anne Kananu kubaini ikiwa amehitimu kuteuliwa kuwa naibu wa gavana.

  • Tags

You can share this post!

Barua ya Kang’ata yawasha moto

WASONGA: Serikali ihalalishe mbinu mbadala za masomo janga...