• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mke ataka mume aliyemshambulia kwa panga na kumpa ulemavu aishi jela milele

Mke ataka mume aliyemshambulia kwa panga na kumpa ulemavu aishi jela milele

NA TITUS OMINDE

Mwathiriwa wa Unyanyasaji wa Kijinsia ambaye mumewe amepatikana na hatia ya kujaribu kumua na mahakama ya Eldoret anataka mshtakiwa afungwe maisha.

Kupitia kwa wakili wa serikali, mwathiriwa huyo aliambia mahakama kuwa kisa hicho kimemfanya kupooza baada ya kushambuliwa kwa panga na mshtakiwa ambaye alimkata kichwani na mikononi.

Licha ya mshtakiwa kuiambia mahakama kuwa amerudiana na mkewe na kujutia kilichotokea, mwathiriwa aliiambia mahakama kuwa huo ulikuwa uongo wa kuhofia kifungo na kuapa kuwa kamwe hatarudiana na mtu ambaye nusura amuue.

“Ninachotaka ni haki, mtu huyu ameniharibia maisha yangu, siwezi kufanya kazi yoyote ya kujikimu kimaisha, anaidanganya mahakama. Mahakama imfunge maisha kama vile upande wa mashtaka ulivyopendekeza,” mwanamke huyo aliambia mahakama alipoulizwa maoni yake kulingana na kujitetea kwa mshtakiwa.

Mshtakiwa, Godrfrey Keter Kipkoech alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la kujaribu kuua kinyume na kifungu cha 220 cha kanuni ya adhabu.

Akiwasilisha ombi hilo, wakili wa serikali Patricia Kirui aliambia mahakama kuwa hukumu inayofaa ambayo mshtakiwa anastahili ni kifungo cha maisha.

“Katika kuhukumu tunaomba hukumu ifaayo ya kifungo cha maisha kwa muujibu wa sheria,” alisema Bi Kirui.

Bi Kirui aliambia mahakama kuwa sheria ya uhalifu inalenga kurejesha utulivu, adabu, usawa wa kijamii katika jamii unaolenga kupunguza viwango vya visa vya dhuluma dhidi ya akina mama katika jamii.

Mahakama iliambiwa kwamba mwathiriwa alikuwa kilema na bado hajapona majeraha aliyoyapata.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa ni kwa neema ya Mungu mwathiriwa alinusurika.

“Ukiangalia nyaraka za matibabu ni kwa neema ya Mungu mwathirika alinusurika kwenye majeraha. Kitendo cha mshtakiwa kinastahili kuadhibiwa na hakipaswi kuidhinishwa,” mwendesha mashtaka aliambia mahakama kupitia wasilisho lake.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka ni kwamba shaka hilo lilikuwa ni la unyanyasaji wa kijinsia ambapo mkosaji alitumia uwezo wake kumdhibiti mwanamke huyo mnyonge asiye na hatia.

Katika kesi hiyo, Geoffrey Keter Kipkoech anasemekana kutekeleza kosa la kujaribu kuua.

Shtaka linasema kuwa mnamo Aprili 20, 2020 katika shule ya upili ya wavulana ya Chebisaas katika Kaunti Ndogo ya Moiben mshtakiwa alijaribu kusababisha kifo cha Margret Jelangat ambaye alikuwa mkewe kimakusudi kwa kumkata vibaya kichwani na mikononi.

Alikanusha shtaka hilo alipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 pesa taslimu.

Hakimu mwandamizi wa Eldoret Peter Areri atatoa uamuzi wake kuhusu kesi hiyo mnamo Novemba 21, 2023 baada ya mshtakiwa kuwasilisha malilio yake kortini.

  • Tags

You can share this post!

Mtaalamu – Wafugaji wakumbatie mbinu mbadala kushusha...

Mambo yamechemka: Mulamwah, Ruth K watangaza wanatarajia...

T L