• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mke wa MCA Trans Nzoia alivyotapeliwa nusu milioni akisaka nafasi za kazi polisi

Mke wa MCA Trans Nzoia alivyotapeliwa nusu milioni akisaka nafasi za kazi polisi

Na EVANS JAOLA

Maafisa wa upelelezi kutoka DCI wamefaulu kunasa washukiwa wa genge la matapeli wanne wanaohangaisha wakazi katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Makachero waliokuwa wanafuatilia genge hilo kwa muda walinasa wanne hao mjini Kakamega baada ya uchunguzi uliochukua miezi kadhaa kubaini jinsi wanavyoibia wakazi pesa.

Washukiwa hao wanadaiwa kutapeli wakazi katika kaunti hiyo akiwemo mke wa Diwani mmoja eneo hilo.

Wanne hao pia wanashukiwa kumtapeli mfugaji katika Kaunti ya Uasin Gishu huku wakijifanya kuwa maafisa wa Mamlaka ya Nyama Nchini (KMC).

DCIO wa kaunti ndogo ya Kwanza George Otieng’ alisema wanne hao waliotambuliwa kama Timothy Shiundu, 36, Paul Karanja, 62, Enock Zakayo Mzee, 62, na Bonface Macheni, 63, wana genge mahiri ambalo limekuwa likiibia wananchi na kwamba watashtakiwa kwa utapeli.

Alisema mmoja wa washukiwa hao, Timothy Shiundu amekuwa akijifanya Kamishna wa Polisi, Karanja akijibeba kama mfanyabiashara wa mifugo, Zakayo naye akijiita daktari mstaafu wa mifugo naye Macheni akijibeba kama mwalimu mstaafu aliye na majukumu maalum kwenye genge hilo.

Shiundu anaaminika kufaulu kuteka akili za wakazi wa Trans Nzoia kupitia mbinu za kijanja na tayari anayo kesi ya kulaghai wanawake watatu Sh1.5 milioni.

Margaret Were, mmoja wa waathiriwa na mkewe Diwani wa Kapomboi Kefa Were aliambia Taifa Dijitali kwamba Shiundu aliahidi kumsaidia kupata nafasi za kazi kwa vijana katika kikosi cha polisi na kile cha jeshi.

“Alituaminisha alipotuambia kwamba yeye ni kamishna wa polisi. Binafsi nilipoteza Sh583,000, rafiki yangu mmoja akapoteza Sh580,000 na mwingine wetu akapoteza Sh250,000,” akahadithia.

Viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na MCA Kefa Were alitaka wakazi kuwa waangalifu ili kuepuka kujipata mikononi mwa wahalifu hao.

“Inasikitisha kwamba kuna watu wanalaghai wananchi kirahisi. Tunataka idara ya upelelezi na mahakama kuharakisha kesi hiyo ili washukiwa wafungwe.”

Mustafa Sugoi, mfugaji kutoka eneo la Cherang’any anahadithia jinsi washukiwa hao walimhadaa awauzie ng’ombe wanne na ndama wawili kwa Sh420,000 ambazo hakuzipokea.

“Hawa watu ni wajanja sana. Hebu fikiria, walikuja nyumbani kwangu wakiongozwa na Timothy Shiundu na kutupatia hundi ambazo tuligundua baadaye kuwa ni feki. Walituambia kwamba wanafanya kazi kwa karibu na KMC na wakatupatia bei nzuri ya mifugo ingawa hatukupokea pesa hizo,” akasema.

Mfugaji mwingine kutoka Ziwa, Kaunti ya Uasin Gishu alituambia kwamba genge hilo pia lilimlaghai kupitia mpango wa kuwauzia mifugo.

“Walikuja na lori lililojaa ng’ombe na kutupatia hundi. Tulipoenda benki ndio tupewe pesa, tuliambiwa zilikuwa feki. Hapo ndio tulibaini tumetapeliwa. Tunaomba kitengo cha usalama kitusaidie kupata pesa zetu,” akasema Bw Tuwei.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke ateketea na kubaki majivu katika mkasa wa moto...

Viongozi Waluo watakiwa ‘waache wivu’ kwa walioteuliwa...

T L