• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Viongozi Waluo watakiwa ‘waache wivu’ kwa walioteuliwa kuhudumu serikalini

Viongozi Waluo watakiwa ‘waache wivu’ kwa walioteuliwa kuhudumu serikalini

CHARLES WASONGA na KNA

KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Seth Ochieng’ Kanga anaendelea kushutumiwa kwa kumshambulia, kwa maneno, Katibu wa Wizara ya Usalama Raymond Omollo.

Diwani wa wadi ya Kolwa ya Kati Kelvin Oraro amemshutumu Kanga na mwenzake, mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Joakim Oketch, almaarufu Swagga, kwa kumshusha hadhi ya afisa huyo wa serikali ya kitaifa, kupitia shutuma za kila mara.

“Kama viongozi, tunawaomba madiwani wenzetu kuwapa heshima maafisa wa serikali kuu walioteuliwa na Rais. Kiranja wetu na mwenyekiti wa kamati ya bajeti hawafai kumshambulia Dkt Omollo kwani wanatuharibia sifa kama viongozi katika bunge la kaunti ya Kisumu,” akasema Bw Oraro.

Aidha, Oraro alitoa wito kwa raia kuwapa heshima viongozi wote walioteuliwa kuhudumu katika ngazi ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.

“Kama Waluo tunafahamu kuwa hatukumpigia Rais Ruto kura lakini ikitokea kwamba tunaweza kupata maendeleo fulani kutoka kwa utawala wake, basi twafaa kuyakumbatia kwa mikono miwili,” akaomba.

Diwani Oraro alikariri wito wake kwa jamii ya Waluo kwamba wawaheshimu mtu yeyote kutoka jamii hiyo aliyeteuliwa kuhudumu katika utawala huu ikiwa watafaidi au la.

Mwanasiasa huyo alisema inasikitisha kuwa Mbw Kanga na Oketch wanapania kujijenga kisiasa kwa kuwarushia viongozi wengine matusi.

Akizungumzi suala hilo diwani wa Nyakach Magharibi Gad Olima alimtaka Dkt Omollo kama kiongozi mchapa kazi ambaye anafaa kupewa nafasi ya kuwahudumia Wakenya.

“Twafahamu fika kwamba hatukuipigia kura serikali ya Kenya Kwanza. Lakini kama raia walipa ushuru, tunapaswa kupata huduma kutoka kwa serikali kuu. Kwa  hivyo hatuwezi kumkana afisa wa hadhi ya juu kama Dkt Omollo aliyeteuliwa atuhudimie kama Wakenya,” akaeleza Bw Olima.

Madiwani hao waliapa kusimama na Katibu huyo wa Wizara ya Usalama na hawataruhusu akosewe heshima na viongozi wachache ambao lengo la ni kujizolea sifa kupitia siasa chafu.

Kwa upande wake, mshirikishi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika kaunti ya Homa Bay Mercy Akenge alitoa wito kwa jamii ya Waluo kujiepusha na siasa chafu na watoe nafasi kwa wale wanaoleta maendeleo kufanya hivyo.

Alisema msimu wa siasa umeisha na huu ni wakati wa maendeleo na kupalilia umoja miongoni mwa wakazi eneo hilo na Kenya kwa ujumla.

  • Tags

You can share this post!

Mke wa MCA Trans Nzoia alivyotapeliwa nusu milioni akisaka...

Tanzania yaambia raia waweke akiba nzuri ya mchele na...

T L