• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
MKU kushirikiana na shule spesheli ya St Patrick’s Thika

MKU kushirikiana na shule spesheli ya St Patrick’s Thika

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) na shule spesheli ya St Patrick’s iliyo na wanafunzi wanaoishi na ulemavu zimefanya ushirikiano wa kufanya kazi pamoja.

Mwalimu mkuu wa shule ya St Patrick’s Bw Jàmes Macharia alitoa ombi kwa chuo hicho kufanya mipango ya kuwasajili wanafunzi katika chuo cha MKU, ili wapate mafunzo zaidi.

Naibu Chansela wa MKU, Profesa Deogratius Jaganyi, alisema ushirikiano wao na shule ya St Patrick’ s utazingatiwa iwezekanavyo.

Mwalimu mkuu wa St Patrick’s Bw Macharia alisema wanafunzi walio na mapungufu watanufaika pakubwa iwapo watasajiliwa katika chuo cha MKU kusomea mafunzo maalum.

Alisema shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu wa kufundisha masomo spesheli.

“Iwapo mkataba wetu utazingatiwa, bila shaka wanafunzi wetu watapiga hatua kubwa kwa masomo yao,” alifafanua Bw Macharia.

Naibu Chansela Prof Jaganyi aliwasilisha hundi ya pesa kiasi cha Sh30,000 kusaidia shule ya St Patrick’s.

Kulingana na msomi huyo, kwa miaka miwili iliyopita, MKU iliwasajili wanafunzi wenye ulemavu wapatao 100 kutoka katika vyuo vingine tofauti.

Dkt Sera Kumari alipewa jukumu la kuwaletea pamoja walemavu walio wanafunzi hata kutoka katika jamii ili kuwe na msimamo mmoja wa kuwashughulikia kwa pamoja.

Mashirika mengine ambayo yametia saini mkataba wa ushirikiano ni kama vile Kilimambogo Blind Trust Association (KBTA), ambalo linawafadhili wanafunzi 24 wanaoishi na ulemavu. Wamewapa vifaa vya kisasa vya kusomea 20 aina ya Orbit Reder.

Prof Jaganyi alisema kuna haja ya kuweka mikataba na mashirika mengine akisema watashirikiana vyema na shule ya St Patrick’s na Shirika la Msalaba Mwekundu na shirika la kimataifa la Lions Club International.

“MKU imepiga hatua kwa kuweka mkataba wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 kwa kufuata mwongozo wa kipengee cha shirika la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu Kuziba Mapengo yaliyopo katika jamii ambacho ni SDG- 10,” alisema Prof Jaganyi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na mkuu wa maswala ya chuo cha MKU Prof Peter Wanderi ambaye alipongeza juhudi zilizoendeshwa na chuo hicho katika kushirikiana na mashirika na taasisi nyinginezo.

You can share this post!

Mbogo ajisifia kazi yake Kisauni asema yeye tosha ugavana

Wakulima wakosa soko kwa zao lenye madini muhimu kwa afya...

T L