• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Mkurupuko wa maradhi ya kuendesha Lamu wazua hofu

Mkurupuko wa maradhi ya kuendesha Lamu wazua hofu

NA KALUME KAZUNGU

KARIBU watu 20, wakiwemo watu wazima na watoto Kisiwani Lamu wamefikishwa hospitalini kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa kuharisha unaoaminika kuchangiwa na maji machafu na mvua kubwa inayonyesha eneo hilo.

Jumla ya watu 5 wamelazwa hospitalini, baada ya kuugua maradhi hayo yenye dalili za kuendesha huku 15 wengine wakitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Mitaa iliyoathiriwa zaidi ni Kashmir, Kandahar, Bombay, Mkomani, Gadeni, Bajuru, Langoni na viunga vyake.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Lamu, Mbarak Bahjaj, alithibitisha tukio hilo la watu kuendesha kisiwani, akihatahadharisha wakazi wote kuzingatia usafi.

Alionya kwamba maradhi hayo yanaweza kuenea kwingine kwa haraka.

“Kutokana na hili, idara ya afya inawasihi wakazi wa Lamu wajilinde na ugonjwa huo kwa kwa kuhakikisha chakula kimepikwa kwa hali ya usafi na kuhifadhiwa vizuri. Pia wanywe maji yaliyochemshwa au kutiwa klorini. Dawa hiyo ya kutibu maji inapatikana katika ofisi za Afya ya umma bila malipo. Pia wanawe mikono kwa maji na sabuni kabla ya kula au kumlisha mtoto na pindi wanapotoka chooni,” akasema Dkt Bahjaj katika ujumbe wake kwa umma.

Kadhalika, Idara ya Afya ya Umma iliwashauri wananchi wa Lamu kutumia choo na kutupa mahali salama nepi za watoto (pampers) au wagonjwa.

Aliongeza: “Ni vyema pia kwenda kwa haraka au kumpeleka mgonjwa hospitalini pindi anapoharisha au kutapika. Wananchi pia wanahimizwa kudumisha usafi wa mazingira. Lazima mkumbuke kuwa kujikinga ni bora kuliko kutibu,” akasema Dkt Bahjaj.

Kwa upande wake, Afisa wa Matangazo wa Idara ya Afya ya Umma kaunti ya Lamu, Ahmed Muhsin, alisema tayari wametia dawa katika visima na vidimbwi vyote vya maji kwenye Mji wa Kale, Lamu na mitaa ya Kashmir, Kandahar na Bombay.

Bw Muhsin aliwataka wakazi kutoa taarifa za visima zaidi ambavyo havijafikiwa ili vitiwe dawa.

Kulingana na Idara ya Afya ya Umma, kati ya watu 20 walio na tatizo la kuharisha, 11 ni watoto ilhali 9 ni watu wazima.

“Tumeanza kuweka dawa aina ya klorini kwenye visima mbalimbali kisiwani Lamu. Visima vingi hapa mjini viko wazi na ni rahisi maji yake kuchanganyika na majitaka yanayoendelea kutapakaa mjini na vichochoroni msimu huu wa mvua kubwa. Ninawasihi wananchi kuzingatia usafi na ikiwezekana visima vifunikwe ili kupunguza uwezekano wa kuenea kwa maradhi,” akashauri.

 

  • Tags

You can share this post!

CJ Koome ahimiza familia kukumbatia Mfumo wa Haki Mbadala...

Gari la nishati ya jua ambalo ukilikumbatia litakupunguzia...

T L