• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Gari la nishati ya jua ambalo ukilikumbatia litakupunguzia gharama ya juu ya mafuta  

Gari la nishati ya jua ambalo ukilikumbatia litakupunguzia gharama ya juu ya mafuta  

NA MARGARET KIMATHI

KWA mbali unapotazama utadhani ni tuk-tuk. Lakini unapokaribia, ndipo utakapokiri kuwa vijana wa Kenya wamejaaliwa maarifa ya kufanya uvumbuzi.

Katika Chuo Anuai cha Kitaifa cha Nyeri, wanafunzi wamefanya kile wanachoamini, kitachangia kupunguza athari za moshi wa magari kutokana na mafuta ya petroli na dizeli.

Gari hilo badala yake linatumia nishati safi ya kawi inayotokana na jua, ambalo ni salama kwa mazingira.

Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Magari, John Chomba anasema gari hilo linategemea nishati ya jua pekee.

Hii ikiwa ni njia moja ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kupanda kwa bei ya mafuta, anatumai kuwa litawapa Wakenya sababu ya kukimbilia magari ya aina hiyo.

Bw Chomba asema gari hilo limeundwa baada ya wanafunzi wake kufanya utafiti kuhusu magari mbalimbali ya humu nchini.

“Tuligundua magari hapa nchini yanazalisha hewa chafu ambayo inaathiri Ozoni na pia afya yetu kama binadamu. Kwa hivyo, tulifikiria kutengeneza gari la kisasa linalotumia nishati ya jua. Gari ambalo halitumii aina yoyote ya mafuta. Ni gari linalopunguza gharama ya uendeshaji na hata umiliki,” alisema Bw Chomba.

Magari yanayotumia nishati ya jua hayaharibu hewa.

Tukihamia katika magari yanayotumia miale ya jua, nchi inaweza kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (climate change) na kupunguza utegemezi wa mafuta.

Bw Chomba asema uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na magari yanayotumia mafuta yenye gharama ya juu nchini Kenya, ndio chanzo cha uvumbuzi huu.

“Gari hili lina swichi mbili. Kwanza tunaliwasha kwa kutumia ufunguo, kisha tunawasha kidhibiti ambacho hubadilisha mkondo hadi kwenye injini. Injini inaponguruma gari huanza kusonga,” anaelezea Bw Chomba.

Gari hili linatumia miale ya jua yenye wati 540 ambayo hubadilishwa kuwa kawi ambayo inahifadhiwa kwenye betri.

Kawi hiyo iliyohifadhiwa, hutumiwa kuwasha injini ya gari na kufanya gari litoke hatua moja hadi nyingine.

Ili kupata nishati, paneli hizo zinawekwa kwenye paa la gari ili kuongeza kawi ya jua.

“Gari hili huwekwa paneli zenye wati 340 na 200 ili kuzalisha umeme, moja kwa moja ambao hubadilishwa na kuhifadhiwa kwenye betri ili kuwasha injini ya gari,” aliongeza Bw Chomba wakati wa mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Gari hili likiwa limehifadhi umeme wa kutosha, linaweza kuenda umbali wa kilomita 100 kwa kasi ya kilomita 60 kwa saa.

Gari hilo lililochukua miezi sita kutengenezwa, lina uwezo wa kubeba mzigo wa kilo 800.

Pia linatumia umeme uliozalishwa na jua wenye thamani ya Sh750, 000.

Hata ingawa ununuzi wa gari hili linalotumia nishati ya jua gharama yake ni ya juu, lina uwezo wa kuokoa gharama za muda mrefu na kuwa lenye manufaa kwa mazingira.

Hatua hii inaligeuza kuwa uwekezaji wa busara na wa kufaa.

“Wakati umewadia kukumbatia teknolojia itakayotunza mazingira na kubadili magari yanayotumia nishati ya jua kwa manufaa ya sayari yetu na vizazi vijavyo,” asema Bw Chomba.

Aidha, taasisi hiyo iliomba serikali ya kaunti na ya kitaifa kuunga mkono mradi huu ikiwa ni njia ya kufungua njia kwa ajili ya uzalishaji wa magari hayo yenye gharama nafuu kwa kututumia nishati ya jua.

“Ikiwa serikali itakubaliana na uvumbuzi huo, tutaweza kutengeneza aina nafuu ya gari ambalo litagharimu Sh500, 000,” aongeza Bw Chomba.

Magari yanayotumia nishati ya jua yanabadilisha sekta ya magari kuwa endelevu kwa mazingira, yenye gharama nafuu, ya kibunifu na yenye matumizi mengi. Kwa hivyo yanashindana vyema na magari ya jadi yanayotumia mafuta. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kawi, uuzaji wa magari ya umeme uliongezeka kwa asilimia 43 mnamo 2020 licha ya athari za janga la COVID-19 ulimwenguni.

Magari hayo yanayotumia kawi ya jua yalichangia asilimia mbili ya mauzo ya magari ya umeme.

Ripoti hiyo yaonyesha kwamba magari yanayotumia kawi ya jua yanaweza kuwa theluthi moja ya usafiri wa barabarani duniani ifikapo mwaka wa 2050, na hivyo kupunguza utoaji wa gesi ya Kaboni.

Kadri nchi nyingi zinavyoelekea kwenye nishati mbadala, teknolojia ya magari yanayotumia nishati ya jua itaendelea kukua.

Haya yanajiri huku taifa la Kenya likilenga kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 32 ifikapo mwaka wa 2030 kwa kukumbatia magari yanayotumia umeme.

Serikali inapanga kuanzisha vituo 1, 000 vya kuchajia magari ili kukuza utengenezaji wa humu nchini wa magari ya umeme.

  • Tags

You can share this post!

Mkurupuko wa maradhi ya kuendesha Lamu wazua hofu

Bwanyenye wa Amerika akashifu serikali ya Ruto kwa kutenga...

T L