• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mnigeria akana kumlaghai raia wa Amerika Sh17 milioni

Mnigeria akana kumlaghai raia wa Amerika Sh17 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Nigeria Jumanne alishtakiwa kwa kumlaghai raia wa Amerika kitita cha Sh17.6m akidai atamuuzia kilo 50 za dhahabu. Yusuf Daniel Masara almaarufu Dkt Ibrahim Sacko alfikishwa mbele ya hakimu mkuu Martha Mutuku.

Alikana alipokea pesa hizo kutoka kwa Elrais Ahmed Mohammed ambaye ni raia wa Amerika. Masara alidaiwa alitekeleza uhalifu huo kati Oktoba 8 2020 na Januari 19 2021.

Wakili Collins Kosewe alimweleza Bi Mutuku kwamba mshtakiwa hakupokea pesa hizo mwenyewe ila zilitumwa kwa akaunti ya wakili.

“Mshtakiwa hakupokea pesa hizi binafsi.Zilitumwa kwa akaunti ya wakili na zingali pale,” Bw Kosewe alidokeza akiomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

Hakimu alifahamishwa mshtakiwa amekuwa akiishi nchini Kenya kwa muda wa miaka sita iliyopita na ameoa.

“Kifungua mimba wa mshtakiwa anasema Loretto Convent na wadogo wake wanasoma katika shule ya msingi iliyoko South B,” Bw Kosewe alisema akiongeza , “ Mshtakiwa amekuwa akishirikiana na polisi kukamilisha uchunguzi.”

Hakimu mkuu Martha Mutuku

Mshtakiwa alikuwa anaripoti kila siku kwa afisi ya mchunguzi wa jinai (DCI) katika kituo cha polisi cha Kilimani kila siku.

Bi Mutuku aliombwa amwachilie raia huyo wa kigeni kwa dhamana ya Sh100,000 kama alivyopewa na mahakama hapo awali.

Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda alisema hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bi Mutuku alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu. Pia aliagizwa amwasilishe raia wa Kenya kumsimamia kama mdhamini kabla ya kuachiliwa kutoka korokoroni.

Kesi itatajwa Machi 3,2021 kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Sonko kuendelea kukaa hospitalini

Wauguzi wamtambua mwizi wa watoto Mama Lucy Hospital