• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Moto wateketeza nyumba za familia 50 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru

Moto wateketeza nyumba za familia 50 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru

NA SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 50 zililazimika kuvumilia baridi kali baada ya nyumba 50 kuteketea katika kisa cha moto usiku wa kuamkia leo Jumatano.

Aidha, mvulana wa umri wa miaka 11 amejeruhiwa baada ya kukatwa mkono na mabati wakati wa kukurukakara za kuzima moto na kuokoa mali.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Owino Road katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, South B, kaunti ndogo ya Starehe jijini Nairobi.

Akiongea na Taifa Leo, chifu wa Landi Mawe, Bw Peter Maroa amesema moto ulianza mwendo wa saa nne na ulianzia kutoka kwa nyumba moja kabla ya kusambaa haraka hadi nyumba nyingine kutokana na kuchochewa na upepo mkali.

Isitoshe, Bw Maroa ameongeza kwamba moto unadaiwa kusababishwa na mshumaa baada ya mpangaji kuacha ukiwaka bila yeyote kuwa ndani ya nyumba alipoondoka kuenda dukani.

“Watu wanasema moto ulisababishwa na mshumaa baada ya mwenye nyumba kuondoka na kuacha nyumba yake bila mtu alipotoka kuelekea katika kioski,” Bw Maroa amesema.

Kando na hayo, licha ya magari ya idara ya zimamoto kutoka kwa serikali ya kaunti kufika eneo hilo, hayakuweza kufika pahala pa tukio kutokana na msongamano wa nyumba.

“Malori ya idara ya zimamoto yameshindwa kufika katika eneo la mkasa baada ya kukosa barabara. Imewalazimu wakazi kushirikiana kubomoa nyumba ili kuzuia moto kuenea zaidi,” mama mmoja anayechuuza samaki akasema.

Nyumba zote zilizoteketea zilikuwa zimejengwa kwa mabati.

Fauka ya hayo, waporaji walitumia fursa hiyo kujinufaisha kupora mali ya watu wakijifanya ni miongoni mwa waokoaji.

“Ukipatia mtu runinga akuwekee mahali salama, alikuwa akienda kabisa usijue ni nani uliyemkabidhi mali yako kutokana na kuchanganyikiwa,” Bw Raymond Omondi amesema.

Polisi wanachunguza kisa hicho.

  • Tags

You can share this post!

Pombe na bangi ilivyochochea mwanamume kuua babake

Manchester City wajinasia huduma za kiungo Mateo Kovacic...

T L