• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Mpango wa MKU kujenga hospitali ya kisasa

Mpango wa MKU kujenga hospitali ya kisasa

Na LAWRENCE ONGARO

MWANZILISHI wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) Prof Simon Gicharu, ana mipango ya kujenga hospitali ya mafunzo, rufaa na utafiti katika chuo hicho.

Tamko lake linajiri siku chache baada ya hafla ya kufuzu kwa wanafunzi 24 wa udaktari katika chuo kikuu hicho.

“Kuna haja ya kuwapa motisha wanafunzi wengi kujiunga na kozi ya udaktari ili pia kuongeza hadhi ya MKU,” alisema Prof Gicharu.

Ikijengwa, hospitali hiyo itahudumia umma kwa ujumla kwa kutoa matibabu ya hali ya juu ikilinganishwa.

Alieleza kuwa ni mradi utakaokuwa wa pili wa kujivunia kuhusu masuala ya afya ikitiliwa maanani kuwa walijenga jumba la maabara na chumba cha kuhifadhi maiti cha kisasa kilichogharimu takribani Sh300 milioni katika hospitali kuu ya Thika Level 5.

Aliwahimiza matajiri waliojaliwa kuwa na fedha kujitokeza na kuongeza taasisi kadha za huduma za afya ili wananchi nao waweze kupata matibabu kwa ada nafuu.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano, katika afisi yake chuoni MKU alipokuwa akifafanua kuhusu jinsi anavyopanga kukiendesha chuo hicho.

Alisema lengo lake kuu ni kuhakikisha kunajengwa hospitali itakayozingatia maswala ya matibabu huku pia ikijihusisha na maswala ya utafiti kuhusu magonjwa sugu yanayogunduliwa kutoka kwa walioathirika kimwili.

Alizidi kufafanua kuwa madaktari 24 kutoka chuo hicho waliofuzu hivi majuzi watapata nafasi ya kuonyesha ujuzi wao wa kutibu wagonjwa baada ya kukamilisha muda wa miaka saba masomoni.

Alisema Baraza la Kusimamia Madaktari nchini – The Kenya Practioners and Dentist Council) – lilitoa kibali kwa MKU kuzindua somo la Shahada ya Udaktari na Upasuaji yaani Bachelor of Surgery (MBchB) mwaka wa 2014.

Alisema kabla ya kupata kibali hicho walilazimika kufuata masharti yote yanayohitajika kwa kuweka vifaa vyote vilivyotakikana.

Aliongeza kusema ya kwamba vifaa vyote vilivyowekwa katika taasisi hiyo ya mafunzo vimekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi wanayoendesha masomo ya taaluma inayohusu afya.

“Sisi ndio chuo cha kwanza chini ya umiliki wa binafsi kupata kibali rasmi kuzindua somo la udaktari na somo la ujuzi wa dawa,” alisema Prof Gicharu.

Hivi majuzi katika ubora wa kuendesha masomo yake iliorodheshwa kwa kupewa asilimia 82 na wataalam wa ukaguzi wa kiafya kutoka Afrika Mashariki na taasisi kuu ya masuala ya afya humu nchni.

Naibu chansela wa chuo hicho Prof Deogratius Jaganyi alisema chuo hicho kitazidi kuzingatia ubora wa hali ya juu.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba wanafunzi wanapokea mafunzo ya hali ya juu ili wakifuzu wawe madaktari wa kutegemewa na wagonjwa popote pale watakapotumwa,” akasema Prof Jaganyi.

You can share this post!

Jamhuri ya Czech yaponda Estonia bila huruma katika mechi...

Guinea na Mali zafuzu kwa fainali za AFCON kutoka Kundi A