• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:06 PM
Msiri wa polisi kwenye kesi ya mauaji ya Willie Kimani alilipwa Sh3,000

Msiri wa polisi kwenye kesi ya mauaji ya Willie Kimani alilipwa Sh3,000

Na RICHARD MUNGUTI

MSIRI wa maafisa wa polisi aliyetumika kumvizia wakili Willie Kimani aliyeuawa pamoja na mteja wake na dereva wa teksi na hatimaye kusafirisha maiti zao kutupwa mtoni alilipwa Sh3,000 na polisi 2016.

Bw Peter Ngugi almaarufu Brown alishangaza mahakama alipoungama kiasi cha pesa kwa kazi yote aliyofanya ya kuwaandama Kimani, Josephat Mwenda na Joseph Muiruri Juni 23, 2016.

“Afisa wa polisi Wilson Kamau alinipigia simu baada ya kupeleka teksi waliyokuwa wameabiri marehemu kuiacha Thindingua Limuru, akitaka niende nikachukue kitu kwa vile sikufanya kazi ya bure,” Bw Ngugi aliungama.

Ngugi anayeshtakiwa pamoja na Inspekta wa Polisi Fredrick Leliman, Koplo Stephen Morogo, Koplo Leonard Maina na Sylvia Wanjohi, alimweleza Jaji Jessie Lesiit kwamba Bw Kamau ndiye alimpa kazi ya kuwaandama wahanga hao.

“Kamau alinipigia simu nikiwa Limuru akitaka nirudi Mlolongo nipokee malipo kwa kazi nzuri niliyofanya ya kuwaandama wahanga hao. Kamau aliniambia nichukue pesa ndani ya gari lake na hatimaye akaninunulia pombe na nyama,” Bw Ngugi aliungama.

Mshtakiwa huyo aliyeingia siku ya pili akijitetea katika kesi ya mauaji inayomkabili alieleza mahakama baada ya kuacha teksi hiyo Limuru jioni hiyo ya Juni 23, 2016, aliagizwa na afisa wa polisi aliyemtambua kwa jina Kamenchu ampeleke mjini Thika.

“Je ulimuuliza Kamenchu mnaenda Thika kufanya nini?” kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku akamuuliza.

“Hapana, sikumuuliza Kamenchu tunaenda kufanya nini Thika,” Bw Ngugi alijibu.

“Kwani ulikuwa mahabusu eti kazi yako ilikuwa kuamriwa nenda Mavoko, twende Thika na kadhalika?” Bw Mutuku alimhoji mshtakiwa.

“Hapana sikuwa mahabusu lakini hakuna raia anayeweza kuthubutu kuuliza afisa wa polisi swali akishatoa amri. Wewe unawaona polisi tu ukicheka nao, huwajui hata!” alijibu Bw Ngugi, huku washtakiwa wenzake, maafisa wa polisi wanaoshika doria, askari jela na wananchi waliokuwa kortini kufuatilia kesi hiyo wakiangua kicheko.

Baada ya kusababisha kicheko, Bw Ngugi alisema Kamenchu aliwaamuru waende Thika lakini “hawakufika Thika bali walielekea mtoni.”

Mshtakiwa alieleza korti Kamenchu alimwelekeza mahala ambapo walisimama karibu na mto kisha akafungua buti ya gari na kutoa ‘mizigo’ na kutupa kwa mto.

“Mizigo iliyokuwa ndani ya magunia ilitupwa ndani ya mto Athi River katika eneo la Donyo Sabuk,” alisema Bw Ngugi.

Mshtakiwa huyo alieleza mahakama gari la pili lililokuwa na migizo (maiti) liliendeshwa na afisa wa polisi Bw Kamau.

Baada ya kutupa maiti hizo mtoni Athi River Bw Ngugi na maafisa wengine saba wa polisi waliokuwa wameandamana walirudi Mlolongo kuendelea na kazi zao hadi siku ile walipokamatwa.

Kufikia sasa maafisa wa polisi waliotajwa kwa jina moja moja Kamenchu, Kamau, Waingo na Mwaniki hawajawahi kukamatwa.

Ngugi alikanusha pendekezo la Bw Mutuku kwamba “ufichuzi wote aliotoa mahakamani jinsi Kimani, Mwenda na Muiruri walivyouawa na maafisa wa polisi ni tungo zake tu na wala hazina ukweli.”

Akijibu Bw Mutuku kuhusu ukweli wa ushahidi wake, Bw Ngugi aliapa kwa jina la Mungu akisema, “Haki ya Mungu nimeeleza hii mahakama ukweli mtupu. Hii mahakama ikigudua nimedanganya nichukuliwe hatua kali.”

Aliendelea kusema, “Ushahidi niliotoa hapa mbele ya Jaji Jessie Lesiit ndio ukweli mtupu.”

Kesi inaendelea.

  • Tags

You can share this post!

Niliitwa kusaidia utekelezaji wa mauaji ya wakili...

Mlipuko wa trela la mafuta waua 77 Haiti

T L